Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mwanza

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123, serikali kupitia Tume ya Madini itaendelea kusimamia ununuzi wa bidhaa na huduma kwa kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa Watanzania.

Kauli hiyo ameitoa jijini hapa jana wakati akifungua kiwanda cha ukarabati wa mitambo ya uchimbaji na uchorongaji kinachoendeshwa chini ya ubia wa kampuni za Sandvik ya Sweden na JC Gears Group Ltd ya Tanzania.

“Kazi kubwa imefanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kunakuwapo na mazingira mazuri ya uwekezaji na hivyo kuvutia ushiriki wa kampuni kubwa za madini katika mnyororo mzima wa thamani kwenye sekta ya madini.

Kwa kuzingatia hilo, amesema serikali ilifanya mabadiliko kwenye sheria ya Madini mwaka 2017 yaliyosababisha kutungwa kwa kanuni za ushirikishaji wa Watanzania za mwaka 2018 ili kuweka usimamizi thabiti wa ushiriki wa Watanzania kwenye sekta ya madini.

“Matunda ya kanuni ni hapa leo kwenye ufunguzi wa kiwanda cha kukarabati mitambo ya hudum za madini kinachomilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Tanzania na ya Sweden. Huu ndio muelekeo ambao serikali itauchukua kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanashiriki katika sekta ya madini.

“Miaka michache iliyopita huduma na bidhaa migodini zilikuwa zinapatikana nje ya nchi kwa asilimia zaidi ya 90, kwa sasa tunaendelea kuwajengea uwezo watanzania ili haya yote yafanyike ndani ya nchi kwa asilimia kubwa,” amesema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa JC Gears Group Ltd, James Makanyaga, amesema mabadiliko ya sheria ya madini yameongeza ushiriki wa Watanzania kwenye uchumi wa kwa kiwango kikubwa na pia yamechochea upatikanaji wa ajira.