Watanzania tukazane kuwekeza kwenye ardhi

Leo ni mwaka mmoja kamili umepita tangu nilipoandika makala hapa safuni yaliyokuwa na kichwa, “Njooni shambani mtajirike”. Ilikuwa ni makala yaliyotoa shime kwa Watanzania kuchangamkia fursa ya uwekezaji kwenye kilimo cha miti.

Katika makala yale niliwaeleza Watanzania upana wa faida ya kuwekeza katika miti ya aina mbalimbali huku nikijikita katika miti ya mbao, karatasi na nguzo. Nilichambua kwa kina gharama za upandaji wa miti hiyo, muda wa kuvuna, soko lake lilivyo na matarajio ya biashara hiyo kwa miaka ya baadaye.

 

Leo ninaandika tena makala haya huku nikiwa na furaha tele moyoni kwa sababu Watanzania wengi waliuitikia mwito wangu na wakachangamkia fursa hii. Kama ambavyo nilitamani iwe, ndivyo ilivyokuwa kwani wengi wamenijulisha kwamba walichangamka na kuanza kuwekeza.

 

Ingawa mimi ni mmoja ya Watanzania wanaojishughulisha na uwekezaji katika mashamba ya miti mkoani Iringa, kiu yangu ilikuwa ni kuona watu wakichangamkia fursa hii mahali popote inapopatikana. Mikoa ya Tanga, Njombe, Mtwara, Tabora, Mbeya, Bukoba na kwingineko kunastawi miti ya aina mbalimbali.

 

Kwa hakika wengi wameendelea kufanya hivyo kwani wamekuwa wakinijulisha. Wapo makumi waliosafiri hadi hapa Iringa kujifunza na kujionea fursa hii inavyowanufaisha na kuwatajirisha watu; kati yao wapo walioamua kuanza kuwekeza na wapo ambao walirudi kwao kujipanga kwa ajili ya kuwekeza wakati ujao.

 

Furaha yangu ilikuwa kubwa zaidi pale nilipoona na kusikia waliofika kujifunza hapa Iringa waliporudi katika maeneo yao walianza kuwekeza. Wapo mamia ambao walizungumza nami kwa simu kutoka maeneo mbalimbali wakiwa wamevutiwa na habari zile.

 

Nami kwa moyo mkunjufu nilishirikishana nao uzoefu wangu na kuwahamasisha waanze hata kama ni kidogo kidogo mahali popote wanapoona inafaa. Ni jambo la kujivunia na la fahari kutamka kwamba makala yale yamekuwa na ‘impact’ kubwa kwa Watanzania wengi waliohamasika kuanza kuwekeza katika miti kule Tanga, Tabora, Mbeya, Mtwara, Morogoro na hapa Iringa.

 

Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara katika makala zangu; ni kwamba muda wa kulalamikalalamika umekwisha. Mazoea na utamaduni wa Watanzania wengi kudhani kwamba tunaonewa wakati wote haujatusaidia mpaka hapa kwa jinsi hii hakuna sababu ya kuendelea nao.

 

Mtindo wa kuishi maisha ya kutaka kuhurumiwa yanatupotezea muda wenye thamani. Tumekuwa tukilalamika kuwa wageni (wanaokuja kwa jina la wawekezaji) wanatupora ardhi; lakini tusichokitafakari ni hiki, “Mimi kama Mtanzania kwa nafsi yangu na kwa uwezo wangu nimefanya nini cha maana katika ardhi ninayoweza kuipata hapa nchini ama ninayomiliki?”

 

Bahati nzuri ni kwamba idadi kubwa ya Watanzania tunafahamu kuwa ardhi ni utajiri; lakini hatufanyi juhudi za makusudi kuuvumbua na kuutumia utajiri huo. Tunayo mamilioni ya hekta za ardhi yenye rutuba na yanayofaa kwa kilimo cha mazao ya aina mbalimbali lakini bidii zetu hazijatosha hata tufike mahali tuseme ardhi haitutoshi.

 

Itakumbukwa kuwa wakati nikiandika makala yale mwaka jana, pia nilizindua kampeni ya kimazingira niliyoibatiza jina la “Green The World And Become Rich”.  Kimsingi kampeni hii nililenga kuwahamasisha Watanzania washiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na wakati huo huo wakitengeneza utajiri.

 

Unapochukua fedha yako na kuwekeza kwenye shamba la miti moja kwa moja unakuwa umetunza mazingira kupitia miti uliyopanda lakini pia usiku na mchana kadiri miti inavyoendelea kukua unakuwa ukitengeneza mamilioni.

 

Hii ni namna moja nzuri ambayo Watanzania tunaweza kuwekeza kwenye ardhi. Leo unapanda miti inakaa miaka saba ama kumi unavuna halafu baada ya hapo ardhi yako unaitafutia matumizi mengine. Si hivyo tu, lakini katika hiki hiki kilimo cha miti; ndani ya shamba lako unaweza kufuga nyuki, ukawa unavuna asali huku ukisubiri kuvuna miti yako.

 

Msukumo wa kuanzisha kampeni hii ya “Green The World And Become Rich” niliupata baada ya kutafakari nafasi walizonazo watu wengi wenye nia ya kuwekeza katika kilimo cha miti na katika ardhi kwa ujumla. Nilifahamu kuwa si rahisi sana kwa mtu kutumia fedha zake kugharimia upandaji wa miti kwa faida moja tu ya kutunza mazingira.

 

Nilijaribu kufikiri namna ya kuongeza thamani; hivyo ilinibidi nifanye kazi ya kuwaelimisha watu mbalimbali mambo mengi kuhusu miti, biashara yake na namna inavyolipa. Ninafahamu kuwa mamia ya wanaoendelea kuwekeza kwenye miti sehemu mbalimbali Tanzania, kufuatia kampeni yangu; wanawekeza kwa mtazamo wa kupata faida kifedha huko mbeleni.

 

Hilo ni jema sana lakini wakati huo huo mimi na wadau wengine wa mazingira tunashangilia kwa sababu mazingira yanaimarika huku watu wakitajirika. Vile vile Nilitambua kuwa wengi wanaweza wasiwe na taarifa sahihi kuhusu kilimo hiki, kwa maana ya maeneo kinakostawi, taratibu za upataji maeneo, lakini kubwa kuliko yote ni namna ya usimamiaji wanapokuwa mbali.

 

Nilifahamu mtu angeweza kujiuliza maswali mengi yakiwamo; “Nitawezaje kumiliki shamba Tabora wakati mimi kikazi nipo Dar es Salaam?” “Nitawezaje kufahamu biashara ya mbao, magogo, pindi ukifika muda wa kuvuna?” “Mbali na faida nitajuaje gharama za uendeshaji na je, nitazimudu?”

 

Katika kampeni hii kulikuwa na majibu yote ambayo kwa wale waliovutiwa kuwekeza Iringa katika maeneo inakowekeza kampuni yangu, nilijitolea kuwapa usaidizi wa kuwatunzia na kuyahudumia mashamba yao. Fursa bado zipo nyingi, Watanzania wenzangu tusilale.

 

Ninapoandika makala haya leo ninatumia wasaa huu kuwakumbusha wale jamaa zangu wa kule Tanga, Tabora, Mbeya na kwingineko walioniahidi kuwa wataanza kuwekeza katika maeneo yao mwakani (mwaka huu).

 

Msimu ndiyo umeanza, kuandaa mashamba, miche na maandalizi mengine. Hapo hapo mlipo fanyeni kitu katika ardhi zenu, wekezeni kwa manufaa yenu na ya watoto wenu, isaidieni dunia kwa kuboresha mazingira yake.

 

Wale waliofika Iringa wengi wao nilikuwa ninawapa zawadi ya nakala ya sheria ya ardhi ya mwaka 1999. Wengine waliokuwa wakiwasiliana nami nilikuwa ninawapa semina fupi kuhusu sheria ya ardhi. Kiujumla sheria hii inatupendelea mno wazawa tofauti na malalamiko mengi ambayo huwa ninayasikia.

 

Pengine Watanzania tuna tatizo katika ubunifu na inapotokea wengine wamebuni tunakuwa wepesi wa kudhani wametuibia. Mathalani, tunaishi na ardhi tusiyoifanyia kazi miaka nenda rudi, akitokea mwekezaji akabuni mradi fulani katika ardhi hiyo; tunaanza kuja juu! Hatujiulizi tulikuwa wapi na kwanini hatukuchangamkia?

 

Kingine kinachotumaliza Watanzania wengi ni ile dhana ya kudhani kuwa kilimo ni utumwa, shamba tunaona ni kwa ajili ya waganga njaa na waliokosa nafasi ya kupata ajira nzuri. Hii ni dhana mbaya na inachangia sana Watanzania kutokuwa na mikakati ya kuitumia ardhi kikamilifu.

 

Hata hivyo, nikiri kuwa wapo Watanzania wanaotambua thamani ya ardhi na kuitumia vizuri kwa uzalishaji na uwekezaji wenye tija. Lakini idadi hiyo haitoshi ukilinganisha na idadi ya wasiotambua nguvu na utajiri wa ardhi ambao wanaendelea kulalamika ugumu wa maisha na waliopoteza tumaini.

 

Jambo jingine linalotumaliza Watanzania ni kutokuwa na maono ya muda mrefu. Wengi wetu tunataka mambo ya papo kwa papo, hatupendi kuangalia mambo ya vipindi virefu mbele. Mfano mzuri ni katika hili la uwekezaji katika ardhi.

 

Mtu anaona ni kupoteza fedha kununua shamba leo ambalo pengine linaweza kuja kutumika miaka ishirini huko baadaye. Mtu anaona ni kama kupoteza fedha kupanda miti leo ambayo atakuja kuivuna miaka saba ama kumi ijayo.

 

Wasichokumbuka wengi ni kuwa unachopuuza kufanya leo kwa gharama ndogo miaka ishirini ama kumi ijayo hutakuwa na uwezo wa kukifanya hata kama ukitamani. Mzee wangu mmoja hapa Iringa alinisimulia namna alivyopuuza kununua kiwanja kimoja hapa mjini Iringa mtaa wa Miyomboni, mwaka 1994.

 

Wakati huo anasema kiwanja hicho kilikuwa kikiuzwa kwa Sh 400,000; lakini mwaka jana kimeuzwa kwa Sh milioni 320! Mzee wangu huyu anasema mwaka huo Sh 400,000 kwake zilikuwa ni hela ndogo sana lakini akapuuza. Leo hii miaka 20 baadaye kiwanja kile kile kimeuzwa mara mia nane ya bei aliyoipuuza ilhali yeye (mzee wangu huyu) leo hana hata ujanja wa kupata Sh milioni 10!

 

Kwa maneno yake anasema, “Ningekuwa na mipango ya muda mrefu katika kuwekeza kwenye viwanja, ardhi na mashamba, leo mimi ningekuwa milionea hapa mjini.” Anachofanya mzee wangu huyu ni utekelezaji wa ule msemo, “Majuto ni mjukuu.”

 

Watanzania tusilale, ushindi wetu kiuchumi umo ardhini!

 

[email protected]

+255 719 127 901