Watu waliokufa kwa tetemeko Uturuki na Syria yafikia 9,000, mbwa wapelekwa

Vikosi vya uokozi nchini Uturuki na Syria wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana na kuiondoa miili zaidi kutoka kwenye vifusi vya maelfu ya majengo yaliyoporomoka kutokana na tetemeko kubwa la ardhi.

Idadi ya vifo imepanda leo na mpaka sasa inakaribia watu 10,000, na kulifanya tetemeko hilo kuwa baya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika zaidi ya muongo mmoja.

Shirika la kushughulikia majanga la Uturuki limesema idadi ya vifo nchini humo imepanfa hadi 6,957, na kufikisha jumla ya watu 9,600, wakiwemo waliokufa katika nchi jirani Syria tangu janga hilo la Jumatatu na matetemeko mengine madogo yaliyofuata.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Syria, idadi ya waliokufa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali imepanda hadi watu 1,250 huku 2,054 wakijeruhiwa.Karibu watu 1,280 wamekufa katika maeneo ya kaskazini magharibi yanayodhibitiwa na waasi.

Wakati huo huo,Mexico imetuma baadhi ya mbwa wake maarufu wa utafutaji na uokoaji nchini Uturuki kusaidia kutafuta watu waliofukiwa chini ya vifusi kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatatu.

Ndege iliyokuwa na mbwa 16 ilipaa kutoka mji wa Mexico City mapema Jumanne.Mexico, ambayo inakabiliwa na matetemeko ya ardhi, ina timu maalum za kiraia na kijeshi ambazo mara nyingi hutumwa kusaidia wakati majanga yanapotokea.

Mbwa hao walivutia mioyo ya watu wa Mexico wakati wa tetemeko la ardhi la 2017 nchini humo, walipookoa maisha ya watu kadhaa.

Mbwa anayeitwa Frida alipata umaarufu kimataifa alipoonekana akiwatafuta manusura katika Jiji la Mexico akiwa amevalia miwani na buti za kujikinga.

Jeshi la wanamaji lilimsifu Frida kwa kuokoa maisha ya watu 12 na kupata miili 40 katika operesheni katika nchi za Mexico, Haiti, Guatemala na Ecuador.

Wakati Frida alikufa kutokana na uzee mwaka jana, angalau mmoja wa mbwa wenzake waliokuweko katika tetemeko la Mexico la mwaka 2017 atakuwa sehemu ya timu ya Navy ya Mexico inayosafiri kwenda Uturuki.

Ecko, mbwa mwenye asili ya Ubelgiji, Malinois, alionekana kwenye uwanja wa ndege wa Mexico City akiwa na mhudumu wake wa jeshi la wanamaji.

Kikundi cha wafanyakazi hao wa kujitolea wenye uzoefu mkubwa walikuwa wamemtumia ujumbe Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico Marcelo Ebrard kutaka kushiriki kutoa msaada wao.

Mexico sio nchi pekee inayotuma mbwa kusaidia katika juhudi za uokoaji nchini Uturuki na Syria. Croatia, Jamhuri ya Czech, Ujerumani, Ugiriki, Libya, Poland, Uswizi, Uingereza na Marekani pia zinapeleka mbwa na wakiwa na waongozaji wao