Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia, Dar es Salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 16 kuhusika na vitendo vya kihalifu ikiwemo kupanga njama za kuiba, kuvunja nyumba huku wengine wakiuuza na kusafirisha dawa za kulevya.

Akizungumza leo Juni 7,2024 Kamanda Kanda Maalumu ya Polisi Dar es salaam SACP Jumanne Muliro amesema Mei 21 2024 maeneo ya Kipunguni B, Ukonga katika msako jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata Hassan Yahya @cobra na wenzake watatu wakitumia dawa za kulevya aina ya bangi huku wakipanga njama za kufanya vitendo vya kihalifu yakiwemo makosa ya unyang’anyi.

SACP Muliro amefafanua kuwa Watuhumiwa hao walikutwa na pistol toy 7, AK47 toy 2, Jambia toy 2, shoka toy 2, kama sehemu ya maandalizi ya kufanya kuhalifu hivyo jeshi la Polisi litaendelea kujikita katika kuzuia matukio ya kihalifu kwa kuafutilia kwa karibu makundi yote ya watu na hasa wanatumia dawa za kulevya na kufanya matukio ya kihalifu.

Sanjari na Operesheni hiyo walifanikiwa kuwakamata jmla ya watuhumiwa 13 wanao husika na kuuza, kusafirisha na kutumia dawa za kulevya ikiwemo bangi wahusika hao ni pamoja na Hamis Seif (18) Mkazi wa Mbondole na Bosco Bosco (18) Mkazi wa Kipunguni Ilala


Watuhumiwa hao wamekamatwa na Puli 531 na kete 2,639 na misokoto 158 ambayo ilikuwa tayari kutumiwa wakiwa pia na viroba vinne vya bangi pia pikipiki mbili MC 673 CKM na MC 591 CUW zilizokuwa zinatumika kusambaza bangi hizo pia zimekamatwa.

Katika hatua nyingine katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Mei 2024 madereva 21 Pikipiki walifikishwa mahakamani na wengine kutozwa faini kuhusika na makosa mbalimbali barabarani ikiwemo kutokuwa na leseni ,kuzidisha abiria, wengine wakiendesha chombo hiko cha moto wakiwa wamelewa.

Pia Madereva wa magari 6 walikamatwa kwa makosa ya kuendesha wakiwa wamelewa ambapo madereva 2 walifikishwa mahakamani na wengine 4 walitozwa faini papo hapo.

Vilevile katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Mei 2024, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam katika kusimamia mifumo ya haki jinai lilifanikiwa kupata matokeo Mahakamani ya watuhumiwa mbalimbali Ikiwa ni pamoja na Agustino Daniel (22) Mkazi wa Vingunguti alihukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kulawiti kwenye Mahakama ya Wilaya Kinyerezi.
Conradi Nnkuru (43) mkazi wa Msongola kwenye Mahakama hiyo hiyo ya Kinyerezi alihukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kubaka makosa mengine Unyang’anyi wa kutumia silaha washtakiwa 3 kwenye Mahakama ya Wilaya Temeke walipata adhabu ya kifungo miaka 30 jela akiwemo Mikidadi Juma (40) mkazi wa Mbagala.

Aidha Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za kweli zitakazo pelekea kukamatwa kwa halifu haraka kabla hawajatekeleza uhalifu wao.