Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wazee nchini kushirikiana kutatua changamoto za mmonyoko wa maadili ili kuwa jamii inayojali usawa.

Aidha amevitaka vyama vinavyoshughulika na masuala ya Wazee nchini kufanya kazi kwa karibu na Mabaraza ya kisera ya Wazee kupitia mwongozo wa Kitaifa uliozinduliwa tarehe 6 Oktoba 2023 kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wazee kitaifa mkoani Geita.

Waziri huyo ameeleza hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Chama cha Wazee Wanaume Tanzania iliyofanyika jijini Dodoma Oktoba 27, 2023,na kueleza kuwa asasi na vyama vyote vya Wazee nchini kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sera, Sheria, Miongozo na Mipango ya Serikali .

Amesema chama hicho pia kina wajibu wa kuchochea Malezi chanya ya Watoto na Vijana, huku wajumbe wa Chama hicho wakiwa mfano kwenye kuwajibika kukemea mmomonyoko wa maadili katika jamii unaosababishwa na kukosa malezi stahiki.

“Kwa asasi na vyama vyote vya Wazee Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano, tunafanya pia juhudi Kuunda mabaraza ya ushauri wa masuala ya wazee ambayo ni kiungo cha kisera kati ya jamii ya wazee wa makundi mbalimbali na Serikali,tunaamini kwa kushirikiana na majukwaa ya wazee tutafanya mapitio ya Sera ya wazee ya mwaka 2003 na kuja na rasimu ya sera mpya ya wazee ya mwaka 2023 ambayo iko kwenye hatua za mwisho, “amesema

Akitoa salaam za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerard Mongela amewataka wazee kuwa sehemu ya kusaidia maendeleo ya nchi kwa kuendelea kuwa washauri wazuri na kuwafungulia mlango vijana wanaotumikia taifa.

Amesema, ” Viongozi vijana wanahitaji sana hekima ya wazee, chini ya Uongozi wa Rais Samia mkawe kielelezo, muendelee kutoa ushauri bila kuchoka. Kupitia Chombo chenu, mtumie taaluma zenu muweke kwenye maandishi ili iwe kumbukumbu” amesema Mongela

Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wazee Wanaume Joseph Laizer amebainisha kwamba Chama hicho kimetokana na kuwa na malalamiko mengi ya kusahaulika kwa wazee hasa katika huduma za afya na maadili.

“Tumeamua kurudi kule tulipotoka, tujaribu kurudisha maadili vijijini, watoto wetu wanaposoma wanabadilika na kusahau jadi yao” amesema Laizer

Kwa upande wake Katibu Mwenenzi wa Chama cha Wazee Wanaume John Sagata akiwasilisha risala ya chama hicho amesema lengo la chama hicho ni kuungana wanaume wazee katika kujadili masuala yanayowahusu ambapo hadi sasa kina jumla ya wanachama 23146 katika mikoa 22 nchini.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma Mchungaji Paulo Mpolo amebainisha kuwa, Baraza la Wazee ndio linabeba wazee wote wa kike na wa kiume hivyo amekiomba chama cha Wazee na vyama vingine vyote kushirikiana katika kuwatetea wazee.

“Kazi ya kutengeneza malezi na maadili yoyote ni kazi ya wazee, tulijisahau tukaacha kuwasaidia watoto wetu juu ya maadili yetu ya Kiafrika. Tuamke sasa na tukatae kuitwa tumepitwa na wakati, tusaidie kizazi chetu.” amesema Mzee Mpolo.