Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amewasimamisha kazi watumishi 11 waliokuwa wakifanya kazi katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Dodoma kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

Hatua hii ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhusu kuboresha huduma za sekta ya ardhi katika halmashauri za Jiji la Dodoma na Mwanza.

Aidha, ameilekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kufanya uchunguzi dhidi ya watumishi hao na kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika.

Silaa ametoa maelekezo hayo jijini hapa leo Oktoba 23, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa hatua hiyo inalenga kuboresha sekta ya ardhi nchini.

Amesema, “Oktoba 3, mwaka huu, Serikali ilitoa maelekezo yaliyolenga kuboresha sekta ya ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Mwanza ambapo wizara imeanza kuchukua hatua ambapo tumewasimamisha kazi watumishi wawili waliokuwa wakifanya kazi Mwanza na watumishi tisa wa Jiji la Dodoma kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili,

Ameongeza kuwa “TAKUKURU imefahamishwa kuendelea kuwachunguza watumishi hao na kuchukua hatua,”.

Katika hatua nyingine Silaa amesema Wizara inaendelea na uboreshaji wa Mifumo ya Kielekroniki wa Kutunza Taarifa za Ardhi (ILMIS) ili kuboresha utoaji wa huduma ikiwemo kurahisisha upatokanaji wa hati milki na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa njia ya mtandao.

Amefafanua kuwa maboresho ya mfumo huo yanatarajiwa kukamilika mwaka huu mwishoni na kusambazwa nchi nzima.

“Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na ofisi ya ardhi waliendesha kliniki maalumu ambapo jumla ya wananchi 3,056 walihudumiwa.Hati milki 1,474 zilitolewa papo hapo na utaratibu huu umekuwa ukitekelezwa nchi nzima.

Pia Waziri Silaa ameilekeza Wizara kuzingatia waraka wa Wizara katika ulipaji wa fidia ambapo unasisitiza kutenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia kabla ya Mthamini Mkuu kujiridhisha na majedwali ya kulipa fidia

Pia amesitisha utaratibu wa upimaji shirikishi katika Jiji la Dodoma na kutoa onyo kwa kamati ya mipango miji na mazingira ya Jiji la Dodoma na kuyasimamia mabalaza ya kata ili yawe na tija katika kushughulikia migogoro ya ardhi nchini.

By Jamhuri