Na Mwandishi Wetu — Jamhuri Media
Dar es Salaam

MTAYARISHAJI wa muziki wa Bongo Fleva, Salmini Maenga, maarufu kwa jina la S2Kizzy au Zombie, anatarajia kuachia albamu yake mpya inayokwenda kwa jina la Virus Oktoba mwaka huu, akiahidi kuleta ubunifu na mabadiliko yatakayoongeza msisimko katika tasnia ya muziki.

Akizungumza na waandishi wa habari,Oktoba 9,2026 Jijini Dar es salaam S2Kizzy amesema albamu hiyo itakuwa na sauti tofauti na mwelekeo mpya wa kimuziki, ikiwa na kazi zilizobeba ubunifu wa kipekee pamoja na mwonekano mpya wa kisanii.

Amesema albamu hiyo inajumuisha ushirikiano na wasanii mbalimbali, wakiwemo Nandy na Mbosso, huku akibainisha kuwa kwa mara ya kwanza amefanya kolabo na Nandy ambayo itapatikana kupitia albamu hiyo.

S2Kizzy, ambaye amejipatia umaarufu mkubwa katika utayarishaji wa nyimbo za Bongo Fleva, amesema ameamua kuachia albamu hiyo baada ya kufanya kazi nyingi zilizopata mafanikio ndani na nje ya nchi.

Amesema kipaji chake cha muziki kilianza tangu akiwa shuleni, na baada ya kuingia katika tasnia hiyo amekuwa akitengeneza midundo (beats) kwa wasanii mbalimbali, huku akichangia pia kuwalea na kuwaendeleza watayarishaji wengine wa muziki.

“Mimi kipaji changu cha muziki kilianzia tangu nikiwa shuleni. Nilipojiunga na soko la muziki, nimewatengenezea wasanii wengi midundo na kuwafundisha watayarishaji wengi chini ya Pluto. Sina kinyongo na yeyote, sipendi majungu, licha ya watu kunichonganisha kupitia mitandao ya kijamii. Ninachoangalia ni kazi yangu na albamu hii mpya,” amesema S2Kizzy.

Aidha, amewataka mashabiki wake kujiandaa na mambo mapya kupitia albamu hiyo, akiahidi kuwa kutakuwa na vitu vya kushtukiza ambavyo huenda hawakutarajia, ikiwemo kuwasikia wasanii mbalimbali wakijaribu mitindo mipya ya muziki.

Amesema anaamini Virus itakuwa kazi yenye upekee kutokana na ubunifu uliotumika katika utayarishaji wake na ushirikiano wa wasanii aliowashirikisha.