Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima (kushoto) akimkaribisha mgeni wake Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba mara baada ya kuwasili Mkoani hapo kwa ziara ya kikazi ya kukagua, kutathmini na kuzungumza na viongozi, kuhusu maeneo yanayopendekezwa kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira na Kufuatilia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi Mazingira ya 2004 katika ngazi za Serikali za Mitaa.

Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akizungumza na viongozi na watendaji katika ngazi mbalimbali Mkoani Mara. Pamoja na mambo mengine Waziri Makamba amewataka kuanzisha kamati za usimamizi wa mazingira katika ngazi za vijiji, vitongoji, Mitaa na Kata.

Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba (kulia) akizungumza na Bw. Madaraka Nyerere mara baada ya kutembelea katika makazi ya Hayati Mwl. Julius Nyerere Wilayani Butiama na kuona namna ya kuhifadhi msitu wa Mwalimu kwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.

Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akiwa na viongozi wa Wilaya na Manispaa akipanda Mlima Mukendo ili kujionea namna ya kuuhifadhi ikiwa ni miongoni mwa maeneo yaliyopendekezwa na Baraza la Madiwani kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.

 

Serikali imesema iko tayari kutangaza katika Gazeti la Serikali msitu wa Mwalimu
Nyerere uliopo Butiama Mkoani Mara kama eneo lindwa kimazingira, kufuatia ahadi
iliyotolewa mwaka jana wakati wa kilele cha Siku ya Mazingira Duniani iliyofanyika
Butiama Mkoani Mara.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira January Makamba mara baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na
mwakilishi wa familia hiyo Bw. Madaraka Nyerere.
Bw. Nyerere amesema kuwa kama familia watafurahi sana kwa eneo hilo kutangazwa
kama eneo lindwa ikiwa ni pamoja na kuweka taratibu za matumizi sahihi ya uvunaji wa
rasilimali ndani ya msitu huo na kutoa zuio kwa baadhi ya shughuli za kibinadamu
isipokuwa kwa kibali maalumu tu.
Akiwa katika mwendelezo wa ziara ya kukagua masuala ya usimamizi na uzingatiaji wa
Sheria ya mazingira nchini, Waziri Makamba amesema kuwa lengo la kuhifadhi baadhi
ya maeneo nchini ni kuhakikisha kuwa yanakuwa na usimamizi endelevu kwa manufaa
ya wote.


Awali akiwa katika Manispaa ya Musoma Mkoani Mara Waziri Makamba ametembelea
Mlima Mukendo uliopo Mtaa wa Nyerere, Kata ya Mukendo na kuridhia ombi wa Baraza
la Madiwani la kuomba msitu huo uhifadhiwe kwa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.
“Nawapongeza sana Uongozi wa Mkoa wa Mara, wao wameenda mbali zaidi kwa
kupitisha azimio hili katika Baraza la Madiwani, hii inatupa sisi msukumo wa kufanya
jambo hili kwa haraka zaidi, sisi kama Serikali tutaleta rasimu ya tangazo la gazeti
mapema iwezekanavyo ili tukubaliane masharti na vigezo tutakavyoweka kabla ya
kulitangaza rasmi katika gazeti la Serikali” Makamba alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Makamba ametoa rai kwa ungozi wa Mkoa wa Mara
haraka iwezekanavyo kupendekeza majina ya maafisa wanaofaa kuteuliwa kuwa
wakaguzi wa mazingira na kuliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira Nchini (NEMC) ndani ya mwezi mmoja kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa
Mazingira walioteuliwa na watakaoteuliwa ili waweze kutekeleza majukumu yao
kikamilifu.
“Mratibu wa Mazingira Kanda ya Ziwa, isipite tarehe 30/09/2018 kabla ya wakaguzi
hawa kupatiwa mafunzo na vitambulisho” Makamba alisisitiza.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima amesema Mkoa wake unalenga
kutekeleza kwa vitendo kampeni ya kuifanya ‘Mara kuwa ya kijani’ na mikakati
waliyojiwekea ni pamoja na kupanda miti milioni 10 ndani ya miaka miwili.
Katika kuunga mkono jitihada kubwa za Mkoa wa Mara katika kampeni ya kupanda miti
Waziri Makamba ameahidi kutoa viriba Milioni Moja vyenye thamani ya Shilingi Milioni 5
na laki 5. Waziri Makamba anaendelea na ziara yake Mkoani Mara kwa kutembelea
Wilaya ya Serengeti.

Please follow and like us:
Pin Share