Na Catherine Sungura-TARURA

Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeendelea kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kuboresha miundombinu ya barabara nchini hususan katika Jiji la Dar es Salaam kupitia utekelezaji wa mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II). 

Uwekezaji huu mkubwa wa zaidi ya Shilingi bilioni 517 unaotekelezwa na TARURA unahusisha ujenzi na uboreshaji wa takribani kilomita 250 za barabara katika Manispaa zote tano za jiji hilo.

Katika utekelezaji wa miradi hiyo, TARURA imeendelea kusimamia kwa karibu ubora wa kazi, kasi ya utekelezaji pamoja na thamani ya fedha (value for money), hali inayodhihirisha weledi na uwezo wa taasisi hiyo katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya miundombinu. 

Kupitia DMDP II, TARURA haijajikita tu katika ujenzi wa barabara za lami na zege bali pia imezingatia miundombinu jumuishi inayohusisha mifereji ya maji ya mvua, njia za waenda kwa miguu, taa za barabarani na alama za usalama barabarani. Mbinu hii shirikishi inalenga kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakidhi mahitaji ya watumiaji wote na kudumu kwa muda mrefu.

Matokeo ya juhudi hizi tayari yanaonekana wazi kwa wananchi. Katika maeneo mbalimbali ya Ubungo, Kinondoni, Ilala, Temeke na Kigamboni, wananchi wamenufaika kwa kuongezeka kwa fursa za kiuchumi, kuimarika kwa biashara, kupungua kwa gharama za usafiri na kuongezeka kwa thamani ya ardhi. Aidha, barabara hizo zimekuwa suluhisho la changamoto za muda mrefu ikiwemo mafuriko, foleni na ugumu wa kufikia huduma za kijamii.

Pamoja na mafanikio hayo, TARURA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda na kutunza miundombinu hiyo. Hata hivyo vitendo vya kibinadamu kama utupaji taka hovyo, uchimbaji holela wa mchanga na matumizi yasiyo sahihi ya barabara vinaweza kuhatarisha uimara wa miundombinu hiyo na kuongeza gharama za matengenezo.

Kwa kutambua hilo, TARURA imeendelea kushirikiana na mamlaka za mitaa katika kuhakikisha usimamizi wa karibu wa miundombinu hiyo unafanyika, sambamba na kuchukua hatua dhidi ya waharibifu. Ushirikiano huu ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uwekezaji huu mkubwa unaleta tija endelevu.

Ni dhahiri kuwa TARURA imeendelea kuwa mhimili mkuu katika utekelezaji wa miradi ya barabara za mijini na vijijini kwa kuzingatia viwango, ubora na mahitaji halisi ya wananchi. Hata hivyo, mafanikio ya jitihada hizi hayataweza kudumu bila ushiriki wa wananchi katika kulinda miundombinu hiyo.

Kwa ujumla, utekelezaji wa DMDP II ni kielelezo cha mafanikio ya usimamizi thabiti wa TARURA katika sekta ya miundombinu. Ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha miundombinu hii inalindwa na kutunzwa ili iendelee kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa taifa.