Serikali imefuta leseni 40 za utafutaji madini ambazo wamiliki wake wameshindwa kuziendeleza licha ya kupewa hati za makosa kutakiwa kurekebisha makosa yaliyobainika. 

Waziri wa Madini Mhe Antony Mavunde (Mb) ametoa tangazo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma katika ofisi za Tume ya Madini tarehe 15 Aprili 2026.

Aidha, ameiagiza Tume ya Madini kufuta leseni hizo na kuendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara za leseni na kuchukua hatua stahiki za kufuta leseni zote ambazo zitabainika kutokuendelezwa.

Amesema kuwa, tarehe 10 Aprili, 2026 Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imetoa hati za makosa kwa leseni nyingine 43 zikikujumuisha leseni 40 za utafutaji

madini na leseni tatu (3) za uchimbaji wa kati wa madini. 

Waziri Mavunde ameielekeza Tume ya Madini kuendelea na zoezi la utoaji wa hati za makosa na endapo wamiliki wake watashindwa kurekebisha makosa ndani ya siku 30, leseni hizo zifutwe ili maeneo hayo yatolewe kwa wawekezaji wengine.

Ameeleza kuwa Serikali imeendelea pia kufuatilia kwa karibu mwenendo wa matukio ya milipuko ya madini ya dhahabu (gold rush) katika maeneo mbalimbali nchini, na kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kulinda usalama, kudumisha utulivu, na kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na kanuni za madini.

Kwa mujibu wa sheria za madini za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, shughuli zozote za uchimbaji madini zinapaswa kufanyika kwa kuzingatia umiliki wa leseni halali.