Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
BARAZA la Madiwani Manispaa ya Kibaha limepitisha bajeti ya jumla ya Sh milioni 700 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua zilizonyesha kwa muda mrefu.
Fedha hizo zinatokana na mgao wa Sh milioni 50 kwa kila kata katika kata 14 za Manispaa hiyo, utekelezaji wake ukitarajiwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha kikanuni cha baraza hilo kilichofanyika Aprili 14, 2026.
Akizungumza katika kikao hicho, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Dkt. Mawazo Nicas, alisema awali ilitengwa milioni 420 ambapo kila kata ilikuwa imetengewa Sh milioni 30, lakini kutokana na hali mbaya ya barabara, baraza limeamua kuongeza fedha hizo hadi kufikia Sh milioni 50 kwa kila kata.
Alieleza licha ya kuwepo kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Manispaa imeona ni vyema kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto hiyo kutokana na uharaka wake.
Dkt. Nicas aliwapongeza madiwani kwa kuridhia bajeti hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa juhudi za ukusanyaji wa mapato zinazoendelea kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Wananchi wetu kilio chao kikubwa ni miundombinu ya barabara, ingawa barabara nyingi zipo chini ya TARURA na TANROADS, kwa hatua hii tuliyoichukua tunaamini maeneo korofi yatapata ufumbuzi,” alibainisha.
Diwani wa Kata ya Sofu, Mashaka Mahande, alieleza fedha hizo zitasaidia kurekebisha barabara zilizoharibika zaidi kipindi cha mvua.
Baadhi ya wakazi wa Mailimoja,Tangini, Tumbi akiwemo Emmanuel Charles, Fatuma Issa na Salehe Ally waliishukuru Manispaa kwa uamuzi huo huku wakisisitiza umuhimu wa usimamizi wa utatuzi wa changamoto ya ubovu wa barabara hasa za ndani.




