Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dosoma
WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imepanga kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya stadi za kazi kwa kutangaza mpango wa kusajili jumla ya vyuo 263 vya mafunzo ya ufundi stadi.
Hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya ufundi nchini ili kuwafikia vijana wengi zaidi katika maeneo ya mijini na vijijini, kwa lengo la kuwaandaa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Hayo yameelezwa jana bungeni na Waziri wa Wizara hiyo,Prof Adolf Mkenda wakati akiwasilisha mapato na matumizi ya Wizara hiyo Kwa mwaka wa fedha 2026-2027.
Waziri Mkenda alisema Serikali itasajili jumla ya vyuo 263 vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, hatua inayolenga kupanua wigo wa elimu ya ufundi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Alisema kati ya hivyo, vyuo vya elimu ya ufundi vitakuwa 45, huku vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi vikifikia 1,066, na shule za sekondari za amali 267.
Prof Mkenda alisema usajili wa vyuo hivyo utaenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya mafunzo na vifaa vya kisasa ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu ya vitendo inayokidhi mahitaji ya sekta mbalimbali.
Aidha, mpango huo unatarajiwa kuongeza fursa za ajira, kujiajiri na kuchochea maendeleo ya uchumi wa viwanda kupitia nguvu kazi yenye ujuzi na ubunifu.



