Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kupeleka furaha na neema kwa watumishi wa umma nchini, kutokana na uamuzi wake wa hivi karibuni wa kuridhia kuwapandisha madaraja watumishi 219,042 ikiwa ni hatua ya kihistoria katika kuimarisha Utumishi wa Umma nchini.
Mhe. Kikwete amesema hayo wakati akizungumza na Maafisa Tawala na RasilimaliWatu , katika mkutano uliofanyika Ukumbi wa AICC, Arusha na kuwakumbusha kutekeleza wajibu wa kuwahudumia watumishi wa umma wenzao ili kuleta furaha miongoni mwao na hatimae wapeleke tabasamu kwa watanzania, kama Mheshimiwa Rais alivyoelekeza.
“Ninawaelekeza mkatimize wajibu wa kuwahudumia watumishi wa umma wenzenu ili wawe na ari na morali ya kuwatumikia wananchi, na kwa kufanya hivyo mtakuwa mnaunga mkono kwa vitendo jitihada na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha maslahi ya Watumishi wa umma nchini yanaendelea kuboreka,” alisisitiza Mhe. Kikwete.
Mhe. Kikwete amefafanua kuwa, upandishaji wa madaraja watumishi 219,042 uliotokana na ridhaa ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na ongezeko la mishahara ya watumishi wa umma (2025): +35.1% , Ongezeko la kima cha chini sekta binafsi (2025/26): +33.4%, utapelekea Sekta mbalimbali kuathiriwa na maboresho haya ikiwemo afya, elimu, kilimo, mawasiliano, usafirishaji, nishati, viwanda, biashara, hoteli, michezo, uvuvi, baharini, madini na utamaduni.
Mhe. Kikwete ameanisha kuwa, Matokeo haya kitakwimu yanaonyesha kasi ya mageuzi ya kiutumishi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa kinara katika uongozi wa kimkakati, ambao umejipambanua kuweka mbele ustawi wa watumishi wa umma na ufanisi wa utendaji kazi wa taasisi za umma nchini.





