Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,
Dar es Salaam
Benki ya CRDB imeendelea na uwekezaji wake wa kimkakati katika masoko mbalimbali ikiwemo Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua inayochangia kuendelea kupata matokeo chanya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza Mei 7, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, katika kongamano maalum la wawekezaji na wadau wa benki hiyo lililobebwa na kaulimbiu ya “Dira ya Pamoja ya Ukuaji”, amesema kongamano hilo linaangazia mafanikio, utendaji wa benki pamoja na namna ushirikiano ulivyoendelea kuleta ukuaji endelevu kwa wateja, wawekezaji na uchumi kwa ujumla.
Dkt. Nsekela amesema uwekezaji wa kimkakati wa CRDB katika masoko mbalimbali umeendelea kuleta matokeo yanayoonekana barani Afrika na kwingineko katika robo ya kwanza ya mwaka 2026.
“Benki ya CRDB inatajwa kuwa miongoni mwa kampuni zenye thamani kubwa zaidi zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ikiwa na thamani ya soko ya Dola za Marekani bilioni 2.8, huku ikiendelea kutoa thamani zaidi kwa wanahisa na wawekezaji wake katika maeneo mbalimbali,” amesema Dkt. Nsekela.
Aidha, amefafanua kuwa CRDB imeendelea kuwa mshirika muhimu katika kukuza biashara ndogo na za kati pamoja na kurahisisha biashara za kuvuka mipaka, hatua inayochochea ukuaji wa sekta binafsi ndani na nje ya Tanzania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank, Neema Mori, amesema benki hiyo itaendelea kulinda na kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa kupitia usimamizi madhubuti, uwajibikaji na maamuzi yenye maono ya muda mrefu.
Prof. Mori amesema CRDB itaendelea kuimarisha mifumo ya utawala bora, usimamizi wa vihatarishi pamoja na uwekezaji wa kimkakati ili kuhakikisha ukuaji endelevu, faida thabiti na kuendelea kuwa taasisi ya kifedha inayoaminika ndani na nje ya Tanzania.
“Niwahakikishie wawekezaji na wadau kuwa msingi wa CRDB Bank unaendelea kuwa imara, wenye dira wazi na uwezo wa kuhimili mabadiliko ya soko huku ikiendelea kuleta matokeo chanya kwa wateja, wanahisa na uchumi kwa ujumla,” amesema Prof. Mori.
Naye Afisa Mwandamizi wa Maendeleo ya Biashara wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Innocent Mbele, amesema CRDB imeendelea kufanya vizuri katika soko hilo kutokana na ukubwa na uimara wa hisa zake.
Amesema DSE imefikia mtaji wa zaidi ya trilioni 33, ambapo zaidi ya trilioni 22 zinatokana na kampuni za ndani ikiwemo CRDB.
“Hii ni chachu kubwa kuonesha kuwa kampuni za ndani zinafanya vizuri, na CRDB ina mchango mkubwa sana katika ukuaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam,” amesema Innocent Mbele.




