Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Darv3s Salaam
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga,amewahimiza wafanyabiashara nchini kutumia fursa ya sera ya “uchumi sifuri” iliyotolewa na China ili kukuza biashara na uchumi wao.
Hayo ameyasema wakati wa mkutano
wa wadau wa biashara kuhusu fursa ya kuuza bidhaa nchini China bila ushuru uliofanyika katika Hotel ya Johari Rotana.
Kapinga amesema serikali imejipanga kuhakikisha wafanyabiashara hawakwami katika mchakato wa kusafirisha mazao na bidhaa kwenda China.
“Punguzeni urasimu, wasaidieni wafanyabiashara na waelekezeni wanapokwama ili waweze kutumia vizuri fursa hii,” amesema Kapinga.
Ameongeza kuwa China imekuwa mshirika mkubwa wa biashara kwa Tanzania kwa muda mrefu, hivyo ni muhimu kuweka mikakati madhubuti ya kuwasaidia wafanyabiashara na kulinda mnyororo wa thamani.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian, amesema kuanzia Mei 1, 2026, China imeanza kutekeleza sera ya “uchumi sifuri” kwa nchi 53 za Afrika zenye ushirikiano wa kidiplomasia na China.
Amesema sera hiyo itasaidia kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania kama korosho, kahawa, pamoja na vito vya thamani katika soko la China.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi amesema serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ya biashara ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.







