πŸ“Œ Afungua Mkutano Mkuu wa Mwaka 2026 wa Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO
β€¨πŸ“Œ Asisitiza utoaji wa taarifa sahihi kwa wateja
β€¨πŸ“Œ Aagiza kuboreshwa kwa maslahi ya watoa huduma kuongeza ufanisi wa utendaji kazi

Na Agnes Njaala, Dodoma

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amewataka Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutumia kwa ufanisi mifumo ya kidigitali na akili mnemba ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia
na kuongeza ufanisi wa huduma na mawasiliano kwa wateja.

Mhe. Makamba amesema hayo Mei 18, 2026 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa hao unaofanyika kwa siku tano katika Ukumbi wa Lavenda Hotel jijini Dodoma ukilenga kutathmini utendaji kazi, kutambua changamoto, kujadili mikakati ya kuboresha huduma kwa wateja na kuimarisha mawasiliano ya kimkakati ndani ya Shirika kwa mwaka ujao wa fedha.

β€œ Sote tunatambua, teknolojia ndiyo msingi wa utoaji huduma wa kisasa hivyo ni wajibu wenu Maafisa Huduma kwa Wateja kuhakikisha mifumo ya kidigitali ikiwemo akili mnemba inatumika kwa ufanisi ili wananchi wapate huduma bora na taarifa sahihi kwa wakati.” amesisita , Mhe. Salome Makamba

Katika hotuba yake, amesema Serikali inatambua jitihada za dhati zinazofanywa na TANESCO katika maboresho yaliyofanyika katika huduma kwa wateja na mawasiliano ya kimkakati kupitia matumizi ya mitandao ya kijamii, makundi ya WhatsApp pamoja na utoaji wa elimu kuhusu matumizi salama ya umeme na Nishati Safi ya kupikia.

Aidha, ameitaka Menejimenti ya TANESCO kuboresha motisha kwa watoa huduma kwa wateja ili kuongeza ari na ufanisi wao kazini kwa kuzingatia kuwa wao ni watendaji wa mstari wa mbele katika kujenga taswira ya Shirika kwa wateja .

β€œ Kwa niaba ya Uongozi wa Wizara, nawapongeza watoa huduma kwa kujituma kwenu. Nimuombe Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kusimamia uboreshaji wa maslahi yao ili waweze kutoa huduma bora na yenye uhakika kwa wateja,” amesema Mhe. Makamba.

Akizungumza kuhusu maboresho ya huduma kwa wateja, amesisitiza umuhimu wa kuongeza ufanisi katika vituo vya huduma kwa wateja (Call Centers) ili kuhakikisha changamoto za wateja zinatatuliwa kwa wakati.

β€œNahimiza ushirikiano madhubuti kati ya TANESCO na wadau mbalimbali ili wateja waweze kupata taarifa sahihi kwa wakati. Aidha, kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha ushirikiano wa ndani kati ya Idara za TEHAMA na Huduma kwa Wateja kwa lengo la kufikia viwango bora zaidi vya utoaji huduma,” ameongeza .

Awali akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO, Dkt. Lucy-Mary Mboma, amesema Bodi inaendelea kuthamini mchango wa Maafisa Huduma kwa Wateja na inatarajia kuona Shirika likiendelea kuimarisha taswira yake kupitia huduma bora na mawasiliano yenye tija.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema Shirika limewekeza katika mifumo rasmi itakayowezesha kuhudumia zaidi ya wateja milioni sita kwa ufanisi mkubwa mara itakapoanza kufanya kazi hivi karibuni. Amesema hatua hiyo pia itasaidia kuokoa takribani shilingi milioni 400 zilizokuwa zikitumika kwenye mifumo ya nje.

β€œ TANESCO itaendelea kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya utoaji huduma ili kuongeza ufanisi, kuhudumia kwa uhakika zaidi ya wateja milioni sita na kupunguza gharama za uendeshaji wa mifumo ya nje.” amebainisha, Bw. Twange.

Mkutano huu wa mwaka wa Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja ni muendelezo wa utamaduni wa taratibu za Shirika wenye tija katika kuboresha utendaji kazi kwa maslahi ya Shirika, wateja na nchi kwa ujumla.