KAMBI ya matibabu ya bure iliyofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, imefanikiwa kutoa huduma kwa wagonjwa zaidi ya 24,871, hatua inayoonyesha mwitikio mkubwa wa wananchi katika kupata huduma za afya za kibingwa na kibobezi.

Idadi hiyo inaonesha mafanikio makubwa ya kambi hiyo iliyowaleta pamoja madaktari bingwa na wabobezi kutoka hospitali na taasisi mbalimbali nchini, wakitoa huduma za uchunguzi, matibabu, vipimo na ushauri wa afya bila malipo kwa wananchi kutoka Arusha na mikoa jirani.

Makonda amesema kuwa,Kambi ya matibabu ya madaktari bingwa imefanikiwa kubaini wananchi 1,930 waliokuwa na shinikizo la juu la damu bila kufahamu hali zao za kiafya, hatua iliyotajwa kuwa muhimu katika kuzuia madhara ya magonjwa yasiyoambukiza kupitia uchunguzi wa mapema.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa kambi hiyo, Mbunge wa Arusha ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema jumla ya wananchi 6,070 walifanyiwa uchunguzi wa shinikizo la damu, ambapo asilimia 65 walibainika kuwa na tatizo hilo.

Amesema kati yao, wananchi 1,930 waligundulika kwa mara ya kwanza kuwa na ugonjwa huo na wataendelea kufuatiliwa na wataalamu wa afya ili kupata matibabu na ushauri unaostahili.
“Matokeo ya kambi hiyo yanaonyesha umuhimu wa wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara badala ya kusubiri kuugua. “amesema Makonda .

Ameeleza kuwa magonjwa mengi yasiyoambukiza hayatoi dalili katika hatua za awali, hivyo uchunguzi wa mapema husaidia kuyaweka chini ya uangalizi na kupunguza hatari ya madhara makubwa.

Aidha, amewataka wananchi kujiunga na bima ya afya ili kuhakikisha wanapata huduma za matibabu wakati wowote wanapozihitaji bila kusubiri uwepo wa kambi maalumu. Alisema bima ya afya ni njia bora ya kuwawezesha wananchi kupata huduma za uchunguzi, matibabu na rufaa kwa wakati, hivyo kupunguza gharama zinazoweza kujitokeza wakati wa dharura.

Katika kipindi cha siku nane za kambi hiyo, wananchi walipata huduma mbalimbali za kibingwa zikiwemo afya ya mama na mtoto, uzazi, watoto, macho, masikio, pua na koo, ngozi, afya ya akili, lishe, magonjwa ya moyo, figo, damu, mfumo wa mkojo pamoja na mfumo wa fahamu. Huduma za upasuaji, ikiwemo upasuaji wa macho kupitia magari maalumu ya upasuaji, pia zilitolewa kwa wananchi waliokuwa na uhitaji.

Makonda amesema jumla ya wataalamu 520 wa afya, wakiwemo madaktari bingwa, madaktari bingwa bobezi, wauguzi na wataalamu wengine, walishiriki kutoa huduma katika kambi hiyo, huku idadi ya watoa huduma wote ikifikia takribani 720.

Amewashukuru wadau na taasisi mbalimbali kwa kushirikiana kufanikisha zoezi hilo ambalo limesogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

Kwa upande wao, wataalamu wa afya walioshiriki katika kambi hiyo walieleza kuwa mwitikio mkubwa wa wananchi unaonesha uelewa unaoongezeka kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa afya.

Walisisitiza kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha wagonjwa wote waliobainika na changamoto mbalimbali za kiafya wanaendelea kufuatiliwa na kupatiwa huduma stahiki ili kuboresha afya na ustawi wa jamii.