Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema utekelezaji wa makubaliano ya maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya chama hicho na CCM si hisani wala zawadi kutoka kwa mamlaka zinazotawala, bali ni wajibu unaotokana na misingi na taratibu maalumu zilizowekwa na pande hizo.
Othman, ambaye ni Makamu wa Kwanza Mstaafu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, aliyasema hayo leo, Agosti 27, 2026, mbele ya viongozi, watendaji, wanachama na wafuasi wa ACT Wazalendo huko Bumbwini, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema taratibu za utekelezaji wa makubaliano hayo zimesainiwa na pande zote zinazohusika katika maridhiano, hivyo hatua inayofuata ni kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa.
“Utekelezaji wa makubaliano haya si hisani wala zawadi kutoka kwa mamlaka zinazotawala, bali ni jambo la wajibu kwa mujibu wa misingi na taratibu tulizokubaliana na kusaini,” alisema Othman.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, alisema Wazanzibari wana kiu ya kuona nchi yao ikiepukana na changamoto mbalimbali, akisisitiza kuwa hawatarudi nyuma katika harakati za kisiasa zinazolenga maridhiano na kuitafutia Zanzibar mamlaka yake kamili.
“Sisi tunajua tunalolitafuta, ndiyo ukaona kila siku Wazanzibari wanazidi kusonga mbele katika harakati za kutafuta nchi yao,” alisema Jussa.
Alisema makubaliano yaliyofikiwa ni sehemu ya juhudi za viongozi wa chama hicho katika kutafuta Zanzibar yenye mamlaka kamili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mstaafu wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji maarufu kama ‘Babu’ Duni, alisema wananchi wamechoshwa na madhila na maafa yanayojitokeza kila baada ya miaka mitano kwa visingizio vya vurugu za uchaguzi.
“Kutokana na hilo tumeingia kwenye mazungumzo ili tuondoe mambo kama haya,” alisema Duni.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe, alisema hana shaka juu ya uwezo wa Mwenyekiti wao wa Taifa katika kupigania haki na kujenga Zanzibar yenye maridhiano.
Wanachama wa ACT Wazalendo Wilaya ya Kaskazini B wamempongeza Othman kwa hatua anazochukua katika kuirejesha Zanzibar katika hali ya umoja na mshikamano, huku wakiahidi kuendelea kuwa pamoja naye na kuunga mkono juhudi za maridhiano ya kisiasa nchini.
Katika ziara hiyo, Othman ameambatana na viongozi na watendaji mbalimbali wa chama hicho, akiwemo Katibu wa Habari na Uenezi, Salim Biman; Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi kupitia ACT Wazalendo, Prof. Omar Fakih Hamad; wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee Taifa, Masoud Khamis















