Na Mwandishi Maalumu , JamhuriMedia,Dar es Salaam

Wananchi wametakiwa kutopuuza uvimbe unaodumu mwilini hususan ule usioambatana na maumivu badala yake wafike katika vituo vya afya kwa uchunguzi huku wakihimizwa kujenga utamaduni wa kutambua dalili za saratani ya mitoki mapema.

Wito huo umetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Crispin Kahesa, katika maadhimisho ya Siku ya Saratani ya Mitoki Duniani iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kahesa ambaye pia ni daktari bingwa wa saratani alisisitiza utambuzi wa mapema wa saratani ya mitoki na kupata matibabu kwa wakati kunaweza kuongeza nafasi ya mgonjwa kupata matokeo mazuri ya matibabu.

Dkt. Kahesa alisema saratani ya mitoki inaweza kumpata mtu yeyote bila kujali jinsia, taaluma au rangi hivyo basi jamii inapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo, dalili zake na vihatarishi pamoja na kuchukua hatua pale inapobaini mabadiliko yanayoweza kuashiria ugonjwa.

Alisema Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa watoa huduma katika ngazi za msingi ili kuongeza uwezo wa kutambua saratani mapema sambamba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kufika hospitalini pale wanapobaini dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa huo.

“Tunatambua kuwa kuna changamoto ikiwemo uchache wa vituo vya saratani lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwajengea uwezo watoa huduma katika ngazi ya msingi ili waweze kugundua saratani mapema”, alisema Dkt. Kahesa.

Kwa upande wa huduma za matibabu Dkt. Kahesa alisema ORCI ina wataalamu wa kutosha pamoja na teknolojia na vifaa vya kisasa vinavyowezesha utoaji wa huduma mbalimbali za saratani kuanzia uchunguzi wa awali hadi kubaini hatua ya ugonjwa.

Alisema mashine za tiba kwa mionzi zimeongezwa huku upatikanaji wa dawa ukifikia asilimia 90 hatua inayolenga kuimarisha huduma kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu.

Aidha Dkt. Kahesa aliwataka wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote huku akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu ambao unaweza kuwa mkubwa kwa mgonjwa na familia yake.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Felician Mshanga Memorial Cancer Foundation, Florian Mshanga alisema wagonjwa wa saratani za mitoki na damu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo hofu, ukosefu wa taarifa sahihi na uhitaji wa msaada wa kisaikolojia.

Alisema baadhi ya wagonjwa huogopa kuwashirikisha wengine kuhusu hali zao kutokana na hofu ya kunyanyapaliwa hivyo basi jamii inapaswa kujenga mazingira ya kuwaunga mkono wagonjwa na familia zao katika safari ya matibabu.

Mshanga alisema taasisi hiyo imejikita katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu saratani, kuhamasisha wanawake kupata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi na jamii kupata chanjo dhidi ya homa ya ini pamoja na kusaidia wagonjwa katika safari yao ya matibabu.

Kwq upande wake Daktari Bingwa wa Saratani za MMtoki Iwa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Salama Idd alisema miongoni mwa dalili zinazoweza kuonekana kwa mtu mwenye saratani ya mitoki ni uvimbe katika maeneo mbalimbali ya mwili ikiwemo shingoni, sehemu ya juu ya mapaja kwa ndani na maeneo mengine.

Alisema jambo la muhimu ni kwa wananchi kutopuuza uvimbe unaodumu kwa muda mrefu hususan ule usioambatana na maumivu bali kufika hospitali kwa uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo chake.

Dkt. Salama alisema hatua ya kufika hospitali mapema ni muhimu kwani saratani ya mitoki inapogundulika katika hatua za awali na mgonjwa kupata matibabu kwa wakati nafasi ya kupata matokeo mazuri ya matibabu huongezeka.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Crispin Kahesa akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya saratani ya Mitoki Duniani iliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.