Na Joseph Mihangwa, JamhuriMedia, Shinyanga

Kama kuna maneno thabiti ya kumwelezea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na maisha yake, ni kwamba hakuwa mtu wa “rangi mbili”. Alikuwa mkweli, mpenda watu na haki, mwenye utu na msimamo.

Hakuwa popo ambaye wanyama wanapowashinda ndege hujiita mnyama, na ndege wanapowashinda wanyama hujiita ndege. Alisimama kwenye alichoamini bila kujigeuza kulingana na upepo wa masilahi.

Mwenye kuongea kwa upole, asiyejifanya, mwenye umbo dogo lakini akili kubwa na kali, Mwalimu alisifika kwa umahiri wa kujenga na kutetea hoja zilizoshiba utafiti, mantiki na maono. Kicheko chake kisichokauka hakikuficha ukali wake katika kutetea ukweli.

Alikuwa rafiki wa kila mtu kasoro wajinga na wapumbavu, wenye kujikweza, wasio na utu na wenye kubeza usawa na haki za binadamu, iwe kimataifa au ndani ya nchi. Aliishi kuyapigania aliyoamini tangu utotoni, shuleni, vyuoni, aliposhika madaraka ya nchi hadi kufariki dunia kwake.

Historia ya maisha yake imejaa matukio yanayoonyesha kwamba alithamini zaidi dhamiri yake kuliko masilahi binafsi, ajira au nafasi yake katika jamii. Pale masilahi na dhamiri vilipoumana, au ujinga ulipotumika kuteteresha msimamo wake, aliachia ngazi badala ya kukubali kuwa popo.

Mwaka 1948, alipokuwa akifundisha Shule ya Sekondari ya Saint Mary’s, iliyomilikiwa na Kanisa Katoliki mjini Tabora, uliendeshwa mdahalo uliowakutanisha na walimu wa Shule ya Sekondari ya Serikali Tabora. Walimu wawili Wazungu walikuwa watetezi wa hoja, huku Mwalimu Nyerere akiwa mpinzani wao.

Mada ilikuwa: “Africa has benefited far more than Europe since the Scramble and Partition of Africa.” Yaani, Afrika imenufaika zaidi kuliko Ulaya tangu kinyang’anyiro cha mataifa ya Ulaya cha kuigawa na kuigawana Afrika.

KWA HABARI ZAIDI ZA KINA SOMA JAMHURI NOVEMBAA 17 -23, 2026