Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri Mchengerwa ataja uwekezaji wa afyahuku Mganga Mkuu, Profesa Bruno Senguya akifichua fursa kwa vijana, wataalamu na taasisi za ndani

Tanzania natarajia kupata fursa mbalimbali za kitaaluma, kiuchumi na kiteknolojia kupitia mpango wa Afrika wa kuimarisha afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto kwa kipindi cha mwaka 2026 hadi 2030 unaolenga pia kuifanya nchi kuwa kitovu cha mafunzo, tafiti na ubadilishanaji wa utaalamu barani humo.

Fursa hizo zinajumuisha mafunzo ya wataalamu wa afya, kubadilishana uzoefu na nchi nyingine, kuimarisha vyuo na hospitali, kuvutia uwekezaji katika sekta ya afya na kuongeza nafasi za ajira na ubunifu kwa vijana.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya kwa kujenga na kuboresha zahanati, vituo vya afya na hospitali ili kupunguza umbali wa wananchi kupata huduma.

Amesema lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na maeneo wanayoishi, huku baadhi ya vituo vya afya vikiimarishwa ili kutoa huduma za upasuaji na huduma nyingine zilizokuwa zikipatikana zaidi katika hospitali kubwa.

Mchengerwa amesema zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanahudumiwa kupitia vituo vya huduma za afya ya msingi, hivyo kuimarishwa kwa ngazi hiyo ni muhimu katika kufanikisha malengo ya kuboresha afya ya mama na mtoto.

Ameeleza kuwa dira ya Afrika ya afya ya mama na mtoto ya mwaka 2026–2030 inalenga kufikia malengo makuu matatu ambayo ni kuondoa uzazi wa nyumbani kwa kuhakikisha wajawazito wanajifungulia katika vituo vya afya chini ya usimamizi wa wataalamu, kumaliza vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika na kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.

Anasema utekelezaji wa dira hiyo utazingatia nguzo kuu tatu ambazo ni uongozi wa kisiasa, ushirikiano na uwajibikaji, uwekezaji katika huduma za afya pamoja na matumizi ya afua zenye ushahidi wa kisayansi kupitia huduma za afya ya msingi.

Ametaja huduma zitakazopewa kipaumbele kuwa ni pamoja na kliniki za wajawazito, uzazi salama, huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga, chanjo, lishe na mifumo ya rufaa.

Katika kuimarisha utekelezaji, Mchengerwa amesema kutakuwa na sekretarieti itakayoratibu mpango huo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tume ya Umoja wa Afrika, Africa CDC na nchi wanachama.

Pia kutakuwa na mfumo wa ufuatiliaji kwa kutumia viashiria saba, ikiwamo tathmini ya vifo vya mama na watoto wachanga ili kubaini sababu na kuchukua hatua za kurekebisha mapungufu yanayojitokeza.

Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza nafasi 60 za awali za mafunzo ya ubingwa katika maeneo muhimu ya afya, yakiwamo ukunga, uzazi, usingizi wakati wa upasuaji na huduma kwa watoto wachanga.

Nafasi hizo ni mwanzo wa mpango mpana wa kuongeza wataalamu wenye ujuzi maalumu, huku idadi ya fursa za mafunzo ikitarajiwa kuongezeka kadiri ushirikiano na upatikanaji wa rasilimali utakavyoruhusu.

Akifafanua namna Tanzania itakavyonufaika na mpango huo Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Senguya amesema fursa hizo hazitaishia kwa wataalamu wa afya pekee, bali zitahusisha taasisi za Serikali, vyuo vikuu, hospitali, vyama vya kitaaluma, asasi za kiraia, sekta binafsi na vijana.

Profesa Senguya amesema taasisi za Serikali zitapata nafasi ya kushirikiana na nchi nyingine katika kubadilishana uzoefu wa sera, mipango na mifumo ya utoaji huduma, hususan huduma za dharura za uzazi, watoto wachanga, chanjo na mifumo ya rufaa.

Ameeleza kuwa wataalamu wa Tanzania watapata fursa ya kwenda kujifunza katika nchi nyingine za Afrika, huku wataalamu kutoka mataifa hayo wakija nchini kujifunza mifumo ambayo Tanzania imefanikiwa kuitekeleza.

Profesa Senguya amesema mabadilishano hayo yataongeza uwezo wa wataalamu na kuimarisha utendaji wa taasisi za afya huku vijana wakipata nafasi ya kujifunza, kushiriki katika afua mbalimbali na kujenga uzoefu wa kimataifa.

Amesema vyuo vikuu, hospitali na taasisi za mafunzo nchini vitakuwa sehemu muhimu ya kutoa mafunzo kwa wataalamu watakaonufaika na nafasi hizo 60 pamoja na mafunzo mengine yatakayofuata.

Huku akitaja vituo vya mafunzo nchini vilivyopata ithibati kupitia ushirikiano wa ExA Health Community kuwa ni miongoni mwa taasisi zitakazoweza kutumika kutoa mafunzo kwa wataalamu kutoka Tanzania na mataifa mengine ya Afrika.

Aidha vyama vya kitaaluma ikiwamo Agota, TAMA na vyama vya wakunga, vina nafasi ya kushiriki katika kutoa mafunzo, ushauri wa kitaalamu, kuandaa miongozo na kubadilishana uzoefu.

Ushirikiano huo utasaidia vyama hivyo kupanua wigo wa shughuli zake kutoka ndani ya Tanzania na kushirikiana na taasisi za kitaaluma katika nchi nyingine za Afrika, hivyo kuongeza uzoefu na uwezo wa kutoa huduma bora.

Kwa upande wa asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali, Profesa Senguya amesema zitapata nafasi ya kushiriki katika uhamasishaji wa jamii, tafiti na utekelezaji wa afua zenye ushahidi, pamoja na kujifunza programu zinazofanikiwa katika mataifa mengine.

Fursa hiyo inaweza kuziwezesha taasisi zilizokua nchini kupata uzoefu wa kufanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania, jambo litakaloongeza uwezo wao wa kitaalamu na kiutendaji.

Sekta binafsi nayo imetajwa kuwa na nafasi ya kushiriki katika uwekezaji wa dawa, vifaa tiba, teknolojia za kidijitali na mifumo ya usafirishaji wa wagonjwa.

Profesa Senguya ameongeza kuwa uwekezaji huo unaweza kuchochea ubunifu na kuongeza ajira kwa vijana kwa kuwa sekta binafsi ni miongoni mwa maeneo yenye nafasi ya kutoa ajira na kukuza ujuzi wa kitaalamu.

Taasisi za utafiti na vyuo vikuu vitapata wigo mpana wa kufanya tafiti katika nchi nyingine za Afrika na kubadilishana maarifa, hatua itakayosaidia kuongeza ubora na ushawishi wa taasisi hizo kimataifa.

Hata hivyo amesisitiza kuwa fursa hizo hazimaanishi fedha, zabuni au nafasi za mafunzo zilizohakikishwa kwa kila mdau, bali ushiriki utategemea mahitaji ya nchi, uwezo wa taasisi, makubaliano na taratibu za utekelezaji.

Uzoefu ambao Tanzania imeupata katika kupunguza vifo vya mama na mtoto unaweza pia kutumika kama msingi wa kujifunza na kuboresha maeneo mengine ya huduma za afya kupitia tafiti na ushirikiano wa kitaalamu.

Profesa Senguya amehimiza kushiriki katika uongozi, maamuzi, uhamasishaji wa afya, ubunifu na matumizi ya teknolojia kutatua changamoto zinazozikabili jamii.

Ushirikiano wa vijana wa Tanzania na wenzao kutoka nchi nyingine utasaidia kubadilishana mawazo, kukuza ubunifu na kuongeza nafasi za kujiajiri kupitia teknolojia na miradi ya kijamii.