MBUNGE wa Muleba Kusini, Oscar Ishengoma amehoji bungeni sababu za watumiaji wa Daraja la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kulipia kila wanapopita, huku watumiaji wa Daraja la Tanzanite yote yakiwa Dar es Salaam hawalipi.

Akijibu swali hilo bungeni leo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema watumiaji wa Daraja la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wanalipia kila wanapopita kwa sababu limejengwa kwa utaratibu wa ubia.

“Watu wa Daraja la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wanalipia kila wanapopita kwa sababu Daraja hili limejengwa kwa utaratibu wa ubia, yaani Public Private Partnership (PPP), ambapo mwekezaji hurudisha fedha zake alizowekeza pamoja na faida kutokana na tozo kwa watumiaji.

“Kwa upande wa Daraja la Tanzanite watumiaji hawalipi kwa sababu daraja hilo limejengwa kwa utaratibu wa kawaida kama uliotumika kujenga madaraja mengine nchini,” amesema Naibu Waziri.