Na Joe Beda, JanhuriMedia, Mara

Katika harakati za kuongeza idadi ya watalii na kipata cha taifa, Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) imeelekeza uongozi wa shirika kutekeleza mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Gofu.

Uwanja kwa ajili ya mchezo huo unaotajwa kupendwa na watu wenye fedha, upo pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti eneo la Fort Ikoma mkoani Mara.

Akizungumza na JAMHURI Digital wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanapa Investment Company Ltd., Dk. Richard Matolo, anasema gharama za ujenzi ni Sh bilioni 9.5 na hadi sasa umekamilika kwa asilimia 65.

Moja kati ya mashimo ya gofu ambayo tayari yamekamilika

“Kazi inaendelea. Tayari viwanja (mashimo) 15 kati ya 18. Uwepo wake utawavutia watalii wapenda michezo na kuwafanya waongeze siku za kukaa nchini,” anasema Dk. Matolo, ambaye ni Mhandisi Mshauri.

Tanzania kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inajipanga kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni tano mwaka huu hadi kufikia milioni nane ifikapo mwaka 2030.

Dk. Matola anasema kwamba ‘bidhaa’ hii mpya ya utalii wa michezo (sports tourism) itakapounganishwa na bidhaa nyingine ya utalii wa majini (water tourism) sambamba na utalii wa wanyama (huu wa kawaida) itaongeza tija kwa shirika na taifa kwa ujumla.

Ujenzi wa uwanja wa gofu pembezoni mwa Senapa ni tunda la wazo la Bodi ya Wadhamini ya TANAPA chini ya Jenerali (mstaafu) George Waitara.

“Bodi ilibuni njia mpya kuvutia na kuendeleza utalii. Mcheza gofu atalala kwenye nyumba ya kifahari, ataelekea Nyatwali (pwani ya Ziwa Victoria), hapo atapata huduma ya usafiri wa boti ya kasi kwenda Kisiwa cha Saa Nane, Rubondo na Burigi Chato. Huu ni utalii wa maji.

“Mtalii huyo huyo anaweza kurudi kwa ndege au barabara hadi uwanja wa gofu Serengeti! Hii ni kuongeza thamani ya mnyororo wa fedha za kigeni na mapato zaidi,” anasema.
Kijiografia, Uwanja wa Gofu Serengeti uko nje ya hifadhi na imefanywa hivyo makusudi kuepusha athari zinazoweza kuukumba uhifadhi na mfumo wa ikolojia wa hifadhi hiyo maarufu duniani.

Utandazaji wa mabomba ya kunyunyizia maji uwanja ukiendelea

Dk. Matolo anasema uhifadhi ni jambo nyeti na kwamba kutoweka kwa viumbe wakubwa na wadogo kunasababisha madhara duniani. Uwanja huu umejengwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na unatarajiwa kuwa wa kipekee duniani – si kwa kuwa uko karibu na hifadhi maarufu duniani, bali pia kwa muundo wake.

“Mradi unatekelezwa katika eneo la ekari 450, utakuwa miongoni mwa viwanja virefu zaidi vya gofu duniani, ukiwa na kilomita 7.065, ambapo mchezaji atatembea kilomita 3.528 kwa mashimo ya ndani na kilomita 3.537 kwa mashimo ya nje,” anasema Dk. Matolo.

Awali, akizungumza eneo la Fort Ikoma wiki iliyopita, mmoja wa wasimamzi wa ujenzi wa uwanja, Zakaria Edward, amesema vikwazo ni miongoni mwa mambo yanayoufanya uwanja wa gofu kuwavutia zaidi wachezaji.

“Nimewahi kucheza gofu katika viwanja vingi, kila kiwanja kina changamoto zake. Uwanja huu una changamoto za ziada; upepo, kwa sababu eneo hili ni la wazi. “Hapa upepo hubadili mwelekeo mara kwa mara. Mbali na upepo, tutaongeza vikwazo vingine kama mabwawa ya maji na vingine kadhaa,” anasema.

Edward, mchezaji wa gofu wa Klabu ya Lugalo ya Dar es Salaam anasema ili uwanja ubaki katika ubora wake, eneo hilo kumejengwa bwawa la maji na visima viwili vitakavyotumika kusambaza maji.Anaamini kuwa watalii watavutiwa na uwanja huo kwa kuwa eneo ulipo wanyamapori kama swala na pundamilia hulikaribia na kuonekana kwa urahisi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANAPA Investment Company Ltd., Dk. Richard Matolo

Katika kuhakikisha gofu inachezwa majira yote ya mwaka, Edward anasema:“Mvua huathiri viwanja vya gofu na tumelizingatia hilo. Hapa kutakuwa na mfumo wa mifereji ya maji kuhakikisha mchezo unaendelea hata baada ya mvua kubwa kunyesha.

”Mradi pia unahusisha jengo la kupumzikia wachezaji (club house) ambalo nalo litajengwa.Pembeni ya Uwanja wa Gofu Serengeti, upo Uwanja wa Ndege wa Fort Ikoma na kwa mujibu wa Dk. Matolo nao ni sehemu ya mradi huo na tayari wageni wanaoshuka na ndege hapo hutembelea eneo la mradi kuona maendeleo ya ujenz

Watalii kutoka Boston, Marekani, Paul na Siri Myers ambao wapo Serengeti kwenye fungate, wanasema watalii wenye uwezo wa kifedha watafurahia kuwapo kwa uwanja wa gofu.

Kwa upande mwingine, wawili hao walionyesha kufurahia mandhari nzuri ya Serengeti na kuahidi kurudi tena nchini kutalii.

Mwongoza watalii, Peter Lyimo, ambaye yupo katika fani hiyo kwa zaidi ya miaka 30 sasa, anasema: “Mwanzilishi wa wazo la kujenga uwanja wa gofu Serengeti anastahili pongezi. Hakuna sehemu nyingine duniani ambapo gofu inachezwa huku ukiona wanyamapori. Tutautangaza uwanja huu ili kuvutia watalii zaidi, hasa wawindaji.”

Uwanja wa Gofu Serengeti una jumla ya ‘par’ (idadi ya juu ya mipigo inayohitajika katika shimo) 72; mashimo ya ndani yana ‘par’ 36 na ya nje ‘par’ 36. Uwanja huu una eneo la mazoezi (range) lenye urefu wa mita 430. Kuna maeneo magumu (rough regions) yenye vizingiti kama milima midogo, mabonde, mabwawa ya mchanga (bunkers), na miinuko midogo.

Eneo lenyewe si tambarare. Takriban miti 3,000 ya aina ya ‘acacia tortilis’ itapandwa kuongeza vizingiti (doglegs). Gofu huhitaji umakini mkubwa wa ubongo ili kutumia ‘par’ chache kufikia shimo.

“Kwa sasa, tunaweka mabomba ya daraja la ‘D’ (PVD) kwa ajili ya mfumo wa kumwagilia, ambayo ni sehemu muhimu ya ujenzi.

“Mabomba haya yana unene wa sentimita 1, kipenyo kutoka inchi 6 hadi 1.7. Majani ya gofu ya aina ya bamunda na mashine maalumu za kukata yatatumika,” anasema Dk. Matolo.
Anasema mbali na uwanja wa ndege wa Fort Ikoma, jengo la mapumziko, nyumba za kifahari, hoteli na miundombinu mingine vitajengwa kwa kushirikiana na wawekezaji ili kuhudumia wachezaji.