Na Moses Ng’wat,JamhuriMedia,Songwe

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe imemuhukumu kuchapwa viboko 24 mkazi wa kijiji cha Msia,Kata ya Chitete, wilayani humo Furaha Maisoni Simkonda, kwa kosa la kujaribu kumbaka mwanafunzi wa darasa la kwanza mwenye umri wa miaka 6 kinyume na kifungo 132(1) (2) a.

Akisoma hukumu hiyo mahakamani hapo Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Shughuli Mwampashe amesema mahakama imemtia hatiani mshitakiwa baada ya kujiridhisha na ushahidi upande wa mashitaka.

Mwampashe amesema mahakama hiyo ilitoa hukumu hiyo ya kuchapwa viboko 24 kwa mujibu wa kifungu cha sharia 160(B) cha sura ya 17 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kwa kuwa mshitakiwa amebainika kuwa na umri wa miaka 18.

Mwampashi amesema vitendo vya ubakaji na ulawiti vimeshamili wilayani humo hivyo adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa watu wote wenye tabia za kuharibu ndoto za watoto.

Akitoa utetezi wake mahakamani hapo mshitaki aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwani hatorudia kutenda kosa kama hilo na atakuwa balozi mwema kwenye jamii.

Awali ilibainishwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Serikali Elibariki Mpinga kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Julai 8, 2022 kwa kumvamia mwanafunzi huyo majira ya saa tano asubuhi wakati akienda shuleni akiwa amevaa sare za shule.

Mpinga amesema wakati mtuhumiwa akijaribu kutaka kumfanyia kitendo cha kingono mtoto huyo aliokolewa na mama mmoja ambaye alisikia kelele kichakani ambako mshitakiwa alikuwa akichunga ng’ombe na mbuzi na kisha kukimbia.

Mpinga amesema kijana huyo alikamatwa Julai 24, 2022 eneo la sokoni kijiji Cha Msia baada ya wananchi wananchi kushirikiana kumkamata baada ya kuwepo kwa taarifa za kijana huyo kufanya jaribio la kumbaka na kufikishwa mahakamani hapo Julai 25,2022.

“Mweshimiwa hakimu naiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mtuhumiwa ili kutoa fundisho kwa watu wengine wanaofanya vitendo hivyo”, amesema Mpinga.

Mmoja wa mashahidi waliotoa ushahidi wao mahakamani hapo Esinati Mtinya aliiambia mahakama hiyo kuwa wakati akienda shambani alisikia sauti kichakani ya mtoto akilia alipoenda alikuta kijana huyo amemuangusha mtoto chini na akiwa amevua suruali mpaka kwenye magoti na alipojaribu kumkamata alishindikana kwa kuwa alimshinda nguvu na kukimbia.

Nje ya mahakama Ofisa Ustawi wa Jamii wilayani humo Tabitha swila amesema vitendo vya ubakaji vimekithiri wilayani humo ambapo kesi zaidi ya tano zimefikishwa mahakamani hapo zikiwepo za ubakaji watoto chini ya miaka 15.