WariobaNA ALFRED LUCAS

Huu kweli ni mwaka wa uchaguzi. Vioja na vitimbi havitaisha mwaka huu.
Lengo la chama cha siasa chochote kile duniani ni kushika dola. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinataka kibaki madarakani, vile vinavyopambana na chama hicho, kadhalika.
Kabla ya msiba mkubwa wa Kapteni John Komba ulioikuta CCM na Taifa kwa ujumla, Jumamosi Februari 28, mwaka huu, moja ya vyombo vikuu vya uamuzi wa chama hicho kiliketi Ikulu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine wakatangaza adhabu. Japo hawakushurutishwa na maazimio manane ya Bunge kwa watuhumiwa waliopata mgawo nwa fedha za akaunti ya escrow, lakini kama chama nacho kikaonesha makucha.
Makada watatu — Andrew Chenge, Profesa Anna Tibaijuka na William Ngeleja — wakaondolewa kwenye vikao vya uamuzi vya chama baada ya kuwatia hatiani wanachama hao kwa kosa la maadili.
Kumbuka, kabla ya adhabu hizo viongozi hao, Chenge alivulikuwa madaraka ya uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulika na fedha na bajeti kama ilivyokuwa kwa Ngeleja aliyekuwa anaongoza Kamati ya Katiba na Sheria.
Kwa upande wa Profesa Tibaijuka, mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete, aliutangazia umma kwamba ni vyema akawaachia nafasi ya uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Tayari viongozi hao wameadhibiwa mara mbili kwa kosa lilelile — kukiuka maadili ya uongozi.
Kwa sasa wanahojiwa na Tume ya Maadili katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam. Makosa ni yaleyale, hatufahamu huko mbele uamuzi wa Tume ambayo mwaka mmoja uliopita ilikwisha kukiri hadharani kwamba maadili ya viongozi wa umma yamefifia.
Kamishna Mkuu wa Tume ya Maadili ya Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda, alipata kusema mwaka jana kwamba kuna ongezeko la mmomonyoko wa maadili kwa watumishi wa umma na kwamba ni tishio kwa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Ni kwamba baadhi ya watumishi wa umma wamekuwa wakipokea rushwa, wakivujisha siri za Serikali, kutumia vibaya rasilimali za umma na baadhi kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.
Ukweli ni kwamba misingi ya maadili inaainisha tabia na mienendo inayopaswa kuzingatiwa na viongozi wa umma wakati anaingia madarakani na anapostaafu. Hivyo, ni kinyume cha maadili ya utumishi wa umma kupokea rushwa au zawadi kwani zawadi yoyote anayopewa kiongozi huzua maswali mengi.
Walipokea mgawo wa escrow, wengi wakiwa ni wanasheria kama Chenge, mbali ya wale majaji wa Mahakama Kuu ni wanasheria wanaofahamu fika kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inawataka kutoomba wala kupokea rushwa au fadhila zenye maslahi ya kiuchumi, na kufafanua kuwa sheria hiyo imeweka kiwango kisichozidi Sh 50,000.
Hii haina tofauti na daktari anayemnyima huduma kwa makusudi mgonjwa fulani katika hospitali ya Serikali na kumwambia wakutane katika kliniki yake eneo jingine. Hakuna ubishi kwamba hii ni sehemu ya uvunjifu wa maadili.
Hairuhusiwi hata siku moja kwa mtumishi wa umma kuvujisha siri za Serikali na kuzipeleka kwa waandishi wa habari na kuharibu taratibu nyingi za kazi za Serikali.
Wakati haya yakifahamika, naona wazi kuwa Watanzania wanapelekwa njiapanda. Nawazungumzia Watanzania wenzangu wanaofuatilia mambo mawili makubwa katika nchi hii.
Wakati mtazamo wa Watanzania wengi kwa sasa ni kwenye kura ya maoni na uchaguzi wa mwaka huu yatakayokuja baadaye kuanzia mwezi ujao, mimi nina la ziada ambalo ni hili la baadhi ya viongozi kuhojiwa.
La uchaguzi hili tungoje wakati mwingine, wakati wake, lakini hili la maadili ya viongozi wa umma haliwezi kupita bila kujadiliwa kwa sababu linafanyika kupitia Katiba ya Tanzania inayotumika sasa, katiba ya mwaka 1977 inayotumika pamoja na marekebisho yake.
Inaelezwa kuwa Katiba hiyo si kali, haiendani na wakati na kutokana na hilo ndipo hapo tulipokuja na wazo, kelele, hamasa, hoja ya kutaka Katiba mpya.
Mchakato wa Katiba mpya umetoka mbali kwa maana ya yaliyofanyika ni makubwa na hadi sasa kurejeshwa tena kwa wananchi kupigiwa kura ama ya “ndiyo” kwa wanaoona iko sahihi, na “hapana” wanaoona tofauti.
Hapo ndipo tunapoona kuwa Watanzania tuko njiapanda. Wamebaki kwenye mtanziko kwelikweli wa ama kubaki na Katiba ya sasa ambayo imeelezwa kuwa ni mbovu au kwenda kwenye mpya, ambayo wakubwa wanasema lazima ipigiwe kura mwezi ujao?
 Bila shaka wanajiuliza, kubaki na Katiba ya sasa maana yake tutaingia kwenye Uchaguzi Mkuu kwa Katiba hiyo na kuendelea kutawaliwa chini ya Katiba hiyo au mpya ambayo imepita katika sheria, Tume ya Jaji Joseph Warioba, kisha Bunge Maalum la Katiba (BMK) la Samwel Sitta au tungoje “mfalme” ajaye tuanze naye upya. Swali je, atapenda jambo hili?
Kilio kikubwa cha Jaji Warioba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ni kwamba Katiba ya BMK imeondoa mambo manne muhimu yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya mageuzi.
Mambo hayo muhimu ambayo ni maadili ya viongozi wa umma, madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na Muungano, hivyo ina tofauti kubwa na rasimu alizotoa.
Kikwazo kikubwa kinachofanya kuonekane kama kuna ugumu ni maridhiano hasa kuhusu Muungano, na hivyo wachambuzi wa mambo wanaona kwamba kama kura basi itapigwa mwakani na hivyo kuendelea na ya sasa, inayolalamikiwa kila kona.
Hili la maadili ya umma linaelezwa na wabobezi wa sheria, hasa masuala haya ya Katiba kwamba limepuuzwa kwani imeripotiwa na Jaji Warioba mara kadhaa kwamba wananchi walitoa maoni mazito kuhusu maadili ndani ya jamii na maadili ya viongozi.
Kutokana na maoni ya wananchi, Tume iliimarisha misingi mikuu ya Taifa iliyo katika Utangulizi wa Rasimu. Misingi iliyo katika Katiba ya sasa ni uhuru, haki, udugu na amani lakini kupitia maoni ya wananchi ikaongezwa misingi mipya ambayo ni utu, usawa, umoja na mshikamano.
Kadhalika, inaripotiwa kuwa wananchi pia walipendekeza tunu za Taifa ziwekwe kwenye Katiba ambazo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa (Kiswahili), lakini BMK ya Sitta imeondoa uadilifu, uzalendo, umoja, uwazi, na uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za Taifa na kuziweka kwenye misingi ya utawala bora.
Unakuwaje mwadilifu bila uzalendo na kuenzi umoja? Unakuwaje mwadilifu bila kufuata miiko ya uongozi kabla ya baadaye kulalamika rushwa na ufisadi, pamoja na fedha za umma kuwekwa kwenye akaunti za benki nje ya nchi?
Katika Bara la Afrika nchi kama Afrika Kusini, Namibia na Kenya zimeweka misingi ya maadili na miiko katika Katiba. Hapa kwetu sheria tulizonazo haziwezi kupambana na rushwa na ufisadi.
Katika mazingira haya, kuna maswali yanaibuka katika kumtendea mtu haki. Ngeleja, Chenge na Profesa Tibaijuka wameondolewa kwenye nafasi zao ndani ya chama, kwenye taasisi zao za Bunge na serikalini huku Katiba inayopendekezwa iking'olewa meno ya uadilifu na miiko ya uongozi, je tutakuwa na Taifa linalofuata misingi ya utawala bora?
Adhabu dhidi ya akina Ngeleja, kwa mtazamo wangu, ni kwamba inachokifanya CCM na Serikali yake ni kusafisha nyota ili ionekane Serikali inafanya kazi ambayo wameiwekea magugu kwenye Katiba inayopendekezwa.
Lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza Jaji Warioba kwa ukomavu wake, pale alipoamua kumzungumzia vyema Kapteni John Komba mara baada ya kifo cha Mbunge huyo wa Mbinga Magharibi kwamba familia, jimbo, Wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla wamepata pigo kwa sababu anajua umahiri na ukada wa marehemu.
Kwangu mie haikuwa sawa hata siku moja kumshambulia Warioba eti kwa sababu ya misimamo, japo wapo kwenye chama kimoja maana Warioba alifanya baadhi ya wabunge kumshambulia kwa matusi ndani ya BMK akifananishwa na waasi wazazi wetu wa kwanza katika Bustani ya Edeni, Adam na Hawa.

By Jamhuri