Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa linafanya uchunguzi kufuatia Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kasanga Michael Royan(31), kudaiwa kujiua kwa kunywa sumu katika nyumba ya kulala wageni.
katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Theopista Mallya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Amesema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 27, majira ya saa 5 asubuhi, katika nyumba ya kulala wageni iliyofahamika kwa jina la Safari Bar iliyopo Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Kamanda Mallya amesema kuwa siku ya tukio afisa upelelezi alipigiwa simu na Benard Wilfred ambaye alijitambulisha kuwa ni mmiliki wa nyumba hiyo ya kulala wageni na kueleza kuwa katika nyumba yake ya kulala wageni kuna mteja ambaye amelala na hajaamka na inaonekana kuwa amepoteza fahamu.

Amesema kuwa baada ya kufika eneo la tukio waliingia katika chumba alichokuwa amelala na kumkimbiza Hospital ya Rufani ya Mkoa ya Sumbawanga ambapo alipokelewa na baada ya uchunguzi wa awali ilibainika kuwa amefariki.

Kamanda Mallya amesema kuwa katika uchunguzi umebainisha kuwa marehemu alikua ni mtumishi wa Serikali katika Idara ya Mahakama katika Mahakama ya Mwanzo na kituo chake lilikuwa ni Mahakama ya Mwanzo Kasanga.

Amesema kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa huenda marehemu alikunywa sumu, lakini baadhi ya viungo vyake vya mwili vimechukuliwa na kupeleka sampuli kwa mkemia mkuu ili kupata majibu sahihi ya chanzo cha kifo chake na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kifo chake.

Amesema kuwa marehemu hakuacha ujumbe wowote hivyo imekua ni vigumu kufahamu sababu za tukio hilo.

By Jamhuri