WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea wanachama wapya 60 kutoka Chama cha Wananchi (CUF) ambao wameamua kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM).
Wanachama hao wamepokelewa jana (Ijumaa, Desemba 29, 2017) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Nkowe kata ya Nkowe, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Kabla ya kuwakabidhi kadi za CCM, Waziri Mkuu alipokea kadi za CUF kutoka kwa vijana saba kwa niaba ya wenzao 60. Vijana hao ni Hamisi Juma, Fatuma Abdallah, Mwajuma Mohammed, Thomas Moto, Zainab Nachiluku, Samia Said na Juma Said.

Vijana hao saba waliokabidhiwa kadi mpya za CCM pamoja na wenzao 53, walikula kiapo cha uaminifu.
Kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Bw. Barnabas Essau wanachama wote ni vijana ambao wanajishughulisha na shughuli mbalimbali na wameridhishwa na utendaji wa Serikali ya awamu ya tano.

Bw. Essau alisema wanachama hao wote wametoka vijiji vya Kipindimbi, Nkowe na Mpumbe.
Novemba 5, mwaka huu, Waziri Mkuu alipokea wanachama 37 kutoka vyama vya CUF na CHADEMA kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mbekenyera, wilayani Ruangwa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 29, 2017.

By Jamhuri