Mzunguko wa kwanza Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara umefikia tamati hivi karibuni. Kuna timu ambazo zimefurahia awamu hiyo ya kwanza ya Ligi kutokana na kufanya vizuri.

Kuna timu nyingine zinaugulia maumivu kutokana na kuambulia vipigo vya mara kwa mara na hivyo kumaliza mzunguko huo zikiwa mkiani, hali ambayo kwa vyovyote vile inawakatisha tamaa washabiki wa timu hizo. Hiki ni kipindi ambacho kila timu inajitafakari  jinsi ya kuanza mzunguko wa pili.

Wakati hayo yakiendelea, Shirikisho la Soka nchini (TFF), kupitia bodi yake ya Ligi ilikaa kikao chake cha kwanza na kuamua kuvifungia viwanja kadhaa hapa nchini kwa kile kilichotajwa kuwa ni vibovu na hivyo haviwezi kutumika katika michezo mbalimbali ya Ligi Kuu na hasa katika ule mzunguko wa pili.

Viwanja vilivyofungiwa ni pamoja na Sokoine (Mbeya), Kaitaba (Bukoba), Jamhuri (Morogoro), Ali Hassan Mwinyi (Tabora), Majimaji (Songea), Mkwakwani (Tanga) na Sheik Amri Abeid (Arusha).

Mambo yaliyotajwa hadi kusababisha viwanja hivyo ambavyo asilimia kubwa vinamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kufikia hatua hiyo ni pamoja na baadhi ya maeneo ya viwanja hivyo kubalishwa matumizi yake. Kuna vilivyotajwa kuwa baadhi ya sehemu zake hutumika kama madarasa ya watoto wa chekechea.

Tatizo kubwa ambalo limegusa karibu kila kiwanja kilichofungiwa ni ubovu wa dimba, yaani sehemu ya kati ya kuchezea mpira. Huu ni uamuzi mzuri wa Bodi ya Ligi kwani inalenga ufanisi. Bila shaka wadau wengi wanaona kuwa huenda spidi ya uongozi mpya TFF ikaleta mafanikio ambayo yamekuwa yakisubiriwa muda mrefu.

Kwa tathmini ya haraharaka, viwanja vingi vinavyotumika katika michezo ya soka hapa Tanzania havina viwango.  Nakumbuka kuna wakati uongozi wa zamani uliwahi kutoa onyo kwa kutaka baadhi ya viwanja kufanyiwa ukarabati kabla ligi kuanza.

Ni kweli kwamba matatizo yaliyotajwa kipindi kile ndiyo haya haya ambayo bodi ya Ligi imeyaona na kuamua kuvifungia viwanja hivi, ili vifanyiwe ukarabati kabla ya mzunguko wa pili kuanza ili viweze kutumika.

Ni kweli kabisa kuwa viwanja hivi vimekuwa vikikusanya fedha kutokana na kufanyika kwa shughuli mbalimbali katika viwanja hivyo. Hali kadhalika, tatizo hili la ubovu wa viwanja umechangiwa na wamiliki kukosa kuwa na wataalamu wa kutunza viwanja.

Suala jingine linalokuja hapa ni kuwa utunzaji wa viwanja unahitaji gharama za hali ya juu. Kitu ambacho Bodi ya Ligi imeshindwa kukiangalia kwa sasa kabla ya kufanya uamuzi ambao lazima utavuruga mipangilio ya baadhi ya timu. Hili halipingiki.

Kwa kawaida kila timu ilikuwa ina sehemu yake iliyozoea kuchezea mechi zake, kwa hiyo endapo baadhi ya viwanja havitatengenezwa ndani ya kipindi kinachotakiwa, ina maana kwamba baadhi ya timu zitalazimika kuhama viwanja vyake.

 

TFF wameshindwa kuangalia hili, kwani kufungia viwanja hivyo kwa wakati huu si suluhisho la maana sana katika kutatua tatizo hilo. Kuna mambo mengi ambayo yalishawahi kuzungumzwa kuhusu suala zima la ubovu wa viwanja.

 

Asilimia kubwa ya wadau wanafahamu kuwa ubovu wa viwanja umekuwa kama ugonjwa sugu ambao haujapatiwa dawa yake. Kwa tafsri ya haraka kuvifungia viwanja katika kipindi hiki ambacho Ligi iko katika kipindi cha mpito si suluhisho tosha.

Kuna wakati wadau mbalimbali walishawahi kutoa mapendekezo mbalimbali kama sehemu ya ushauri, jinsi ambavyo tatizo hili linaweza kutatuliwa.

Kuna waliosema kuwa moja ya mambo yanayoharibu viwanja vya soka hapa nchini ni matumizi mabaya ya viwanja hivyo. Hali kadhalika, wengine wakasema kwamba kuna matumizi mabaya ya fedha ambayo imekuwa ikilipwa kwa wamiliki wa viwanja hivyo pale vinapotumika katika shughuli mbalimbali.

Lakini pia kuna waliokwenda mbali zaidi na kusema kuwa kuna haja ya TFF kuingia ubia na wamiliki wa viwanja hivyo, kwani wao ndiyo wenye utaalamu wa kufahamu zaidi vigezo vya kiwanja bora cha soka. Haya ni mawazo ambayo yalishawahi kutolewa.

Kitendo cha Bodi ya Ligi kuamua kuvifungia viwanja hivyo kinaleta maswali mengi kwa wadau wa soka. Kuna viwanja ambavyo vinahitaji marekebisho ya muda mrefu kutokana na uchakavu wake.

Kwanini bodi hii, ambayo mimi nathubutu kusema kuwa iko makini, isingesubiri Ligi ya msimu huu ikaisha halafu ikakunjua makucha yake katika kushughulikia suala zima la viwanja?

Inapofikia hatua hii kuna haja ya kuwashirikisha baadhi ya viongozi ambao wamekuwapo muda mrefu ndani ya TFF, ili nao watoe mawazo yao ambayo yanaweza kuelezea chanzo cha tatizo hili la viwanja ambalo limekuwa la muda mrefu.

Siku hizi biashara imekuwa ya soko huria. Hivi leo wamiliki wa viwanja wakiamua kutumia viwanja hivyo kwa matamasha ya burudani peke yake na wakaachana na masuala ya soka, nani atapata wakati mgumu wa kuongoza soka hili la Tanzania?

Kila awamu ya Serikali ina taratibu zake pale inapoingia madarakani. Uongozi mpya wa TFF unaweza kuwa na mipango mingi yenye lengo la kuendeleza soka la hapa nchini. Kinachotakiwa ni kufikiria na usikivu ili kuzingatia maslahi ya pande zote.

1176 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!