Na Bashir Yakub

Wako wasimamizi wa mirathi wa aina mbili. Kwanza ni yule ambaye marehemu mwenyewe amemteua kabla ya kufa kwake na akaandika/kusema kwenye wosia kuwa fulani ndiye  atakayesimamia  mirathi  yangu  baada  ya  kuondoka.

Pili, ni yule ambaye  hakuteuliwa  na  marehemu mwenyewe bali  ameteuliwa na wanafamilia kwenye kikao  cha  familia. Kwa walio wengi  huyu  ndiye  tunamjua kuwa ni lazima jina lake lipelekwe  mahakamani  kwa  ajili  ya  kuthibitishwa  ili  aweze kuwa  msimamizi  kamili.  Makala itapitia Sheria  ya  Usimamizi  wa Mirathi, Sura ya 352  na kanuni zake.

1.   HAKI NA WAJIBU WA WASIMAMIZI WA MIRATHI

Haki  na  wajibu  wa  msimamia  mirathi  aliyeteuliwa  na  marehemu kabla ya kifo na  ambaye  hakuteuliwa na marehemu ni  sawa. Awe  aliteuliwa  na  marehemu  mwenyewe  au  aliteuliwa  na  wanafamilia  bado  haki  na wajibu  alionao  ni  ule ule.  

Wajibu  mkuu  wa  msimamia  mirathi  ni  kuwa  mwadilifu, na  kuenenda  kwa  mujibu  wa  sheria  katika  kila  hatua  anayopiga katika  kusimamia  kwake  mirathi.

2.   SIO LAZIMA MSIMAMIZI WA MIRATHI AWE NDUGU/MWANAFAMILIA

Hili ni  muhimu  zaidi  kulieleza.  Siyo  kweli  kuwa  msimamizi wa  mirathi  lazima awe mtoto  wa  marehemu, shangazi, baba  mdogo au mkubwa,  mjomba, kaka, dada n.k.  Bali  msimamizi  wa  mirathi  anaweza  kuwa yeyote.  Suala  la  msingi  ni  atimize  sifa  za  kuwa  msimamizi  wa  mirathi. Na katika sifa hamna undugu.

Hakuna  haja  ya  kuwa  na  ugomvi  kuwa  msimamizi  wa  mirathi  lazima  atoke  katika  familia. Hakuna  ulazima  huo  ikiwa  mmeshindwa  kuaminiana  kwenye  familia. Mnaweza  kumteua  hata  kiongozi  wa  dini au  mtu  mwingine  yeyote  mwadilifu  ambaye  mnadhani  ataweza  kutenda  haki  katika usimamizi.

Jambo  jingine,  msimamizi  wa  mirathi  siyo  lazima  awe  mmoja. Ikiwa  kuna  pande mbili  zinazozana,  basi  sheria  inaruhusu  kila  upande  kutoa  msimamizi  wa  mirathi  ili  alinde  maslahi  ya  upande  wake.  Kwa hiyo, wasimamizi watakuwa  wawili   na  sheria  haikatazi.

Nyongeza ya  hapo ni kuwa hata kampuni  au taasisi  inaweza kuteuliwa kusimamia mirathi.

3. MSIMAMIZI ALIYETEULIWA  KATIKA WOSIA  KUTHIBITISHWA NA MAHAKAMA

Msimamizi  aliyeteuliwa  katika  wosia  naye  ni  lazima  kuthibitishwa  na  Mahakama.  Siyo  kwamba  kwa kuwa  marehemu  kabla  ya kufa  alimteua  au kwa sababu  ameandikwa  kwenye  wosia kama  msimamizi  wa  mirathi,  basi  haina  haja  ya  kwenda  tena  mahakamani.

Ni  kweli  aliteuliwa  na  marehemu  kabla  ya  kifo,  lakini  athibitishwe  na  Mahakama. Hivyo  ndivyo  sura ya 352 inavyosema

Ikiwa  hatathibitishwa  na  Mahakama, basi  hawezi  kusimamia mirathi. Lazima awe na fomu  ya  usimamizi  wa  mirathi  itolewayo  na  Mahakama.

Fomu hii  ndiyo  inayoruhusu  kuuza  mali,  inaruhusu  kudai  madeni, unaweza  kuonesha  benki  na  akaunti  za  marehemu  zikafunguliwa  ili  mchukue  hela, inaoneshwa  kwenye kampuni  kama  kuna  hisa  ili kuweza  kupewa  hisa  za  marehemu nk. Huwezi  kuonesha  wosia   ukaruhusiwa  kufanya  miamala  kama  hii.

Kuhusu  sheria  za  ardhi, mirathi, makampuni, ndoa  n.k, tembelea  SHERIA   YAKUB   BLOG.

By Jamhuri