Na MayLoyce Mpombo,JamhuriMedia,Kinyerezi

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kuzalisha umeme inayoitekeleza kupitia TANESCO ambayo inakwenda kuondoa changamoto za umeme na kukuza uchumi wa nchi.

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dunstan Kitandula (Mbunge) wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia cha Kinyerezi 1 Jumamosi, tarehe 18 Machi, 2023 mkoani Dar Es Salaam utakaozalisha jumla ya megawati 185.

Meneja wa Mradi, Mha. Abdallah Chikoyo akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walipotembelea mradi wa kituo cha upanuzi cha kuzalisha umeme kwa gesi asilia cha Kinyerezi (Kinyerezi I Extension) siku ya Jumamosi, 18 Machi, 2023.

“Kama Kamati tumeona mradi unaendelea vizuri na mitambo mitatu tayari imeanza kuzalisha megawati 135 bado mtambo mmoja ambao utekelezaji wake unaendelea vizuri” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati,Stephen Byabato amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa pesa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Jumla ya pesa zitakazotumika hadi mradi huu ukamilike ni dola za kimarekani milioni 188, na hizi ni jitihada zake Mheshimiwa Rais na kwa ufadhili huu tuna uhakika utaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na wenye ubora na kuwezesha maendeleo mbalimbali kwenye viwanda vikubwa na vidogo na maendeleo ya kijamii” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,Maharage Chande alieleza kuwa mradi umepiga hatua kubwa tangu ulipoanza mwaka jana 2022 na mitambo mitatu kati ya minne ipo tayari na imeshaingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa

Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato akiongea mbele za waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini walipotembelea kituo cha upanuzi cha kuzalisha umeme kwa gesi asilia cha Kinyerezi (Kinyerezi I Extension) siku ya Jumamosi, 18 Machi, 2023

“Ifikapo mwishoni mwa Aprili 2023 mtambo wa nne utakuwa tayari kuanza kuzalisha umeme. Hivyo natumia fursa hii kuwashukuru wateja kwa uvumilivu wakati huu mradi unaendelea kujengwa na nawapongeza wafanyakazi kwa kazi ngumu yenye kuleta mafanikio kwa taifa letu” alisisitiza Chande.

Aidha, wajumbe wa Kamati hiyo Consatine Kanyasu (Mbunge) na Jesca David Kishoa (Mbunge viti maalum) wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa hatua zilizofikiwa kwenye mradi huu na wameiomba Serikali kutia mkazo kwenye kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande akizungumzia mradi wa kituo cha upanuzi cha kuzalisha umeme kwa gesi asilia cha Kinyerezi (Kinyerezi I Extension) wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipokitembelea kituo hicho siku ya Jumamosi, 18 Machi 2023.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Kitandula (Mbunge) akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo ilipokitembelea kituo cha upanuzi cha kuzalisha umeme kwa gesi asilia cha Kinyerezi (Kinyerezi I Extension) siku ya Jumamosi, 18 Machi 2023.