Na OWM, Milan Italia.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea shamba la ufugaji wa ng’ombe wa maziwa la Alesandra lilipo Milan nchini Italia, ambalo linaendeshwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kielektoniki ikiwemo ukamuaji wa maziwa kwa kutumia roboti.

Akiwa katika shamba lenye takribani ngombe 500 Mheshimiwa Majaliwa ameshuhudia mifumo bora ya ufugaji, ulishaji , unyonyeshaji na ukamuaji wa maziwa, ambapo ng’ombe mmoja anauwezo wa kutoa lita kuanzia 35 hadi 70 kwa siku na kumuwezesha mfugaji kupata tija zaidi.

Waziri Mkuu alitembelea shamba hilo jana (Alhamisi, Oktoba 19, 2023) na alionesha kufurahishwa na teknolojia inayotumika katika ufugaji huo.

Viongozi wengine walioambatana na Mheshiwa waziri Mkuu kutembelea shmba hilo shamba hilo ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi ambaye alisema amefurahishwa na misingi bora ya ufugaji na kwamba utaratibu huo ukitumika nchini utaongeza tija katika sekta ya mifugo.

SOMA PIA;

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema amefurahishwa na namna ya uendeshaji katika shamba hilo ambalo pia wanafanya kilimo mseto kwa kufuga, kulima malisho ya mifugo na kutumia kinyesi cha ng’ombe kuzalisha nishati ambayo wanaitumia kwa shughuli za shambani na ziada kuuza kwenye gridi ya Taifa.

Alisema jambo jingine lililomfurahisha katika shamba hilo ni namna ambavyo mifugo yao imewekewa hereni za kielektroniki kwa ajili ya utambuzi ambazo zinaiwezesha nchini kujua idadi ya ng’ombe pamoja na maendeleo yake ikiwemo kutambua magonjwa, hivyo atakutana viongozi wa sekta husika ili kuangalia namna bora ya kuboresha ufugaji nchini.

Naye, mfugali wa ng’ombe kutoka Wami Sokoine, Morogoro, Mainga Ole Kalaita ambaye alitembelea shamba hilo kwa ajili ya kujifunza ufugaji bora alisema amepata elimu ya ufugaji bora na atakwenda kuwashauri wafugaji wenzake nchini wabadilike ili waendane na mahitaji ya sasa ya soko ikiwa ni pamoja na kubadili njia za ufugaji. “Hakuna haja ya kuwa na mifugo mingi isiyokuwa na tija, tubadilike tufuge kisasa.”

By Jamhuri