Katika siku za karibuni kumekuwapo na malumbano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Malumbano hayo yalitokana na kada wa Chadema, David Djumbe, aliyepitishwa na NEC kuwania kiti hicho, kuwasilisha barua ya kujitoa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 13 mwakani pamoja na katika majimbo ya Longido na Songea Mjini.

Malumbano hayo yamezidi baada ya kada huyo kuwasilisha barua ya kiapo cha Mahakama kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo ya kujitoa na kukataliwa.

Katika malumbano hayo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, amemtaka Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima, kutojigeuza kuwa msemaji wa chama hicho.

Wakati Chadema wakitoa kauli hiyo, NEC imeendelea  na msimamo wa kumtambua mgombea huyo kuwa ni halali aliyetimiza masharti ya kushiriki uchaguzi.

Katika maelezo yake, NEC imesema kwa mujibu wa ibara ya 67 ibara ndogo ya 1b ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mgombea ubunge lazima awe amependekezwa na chama cha siasa kilichosajiliwa.

Imesema  kwa mujibu wa kanuni namba 31, kanuni ndogo ya kwanza ya uchaguzi wa Rais na wabunge ya mwaka 2015, mgombea atawasilisha barua yake ya utambulisho iliyosainiwa na katibu wa chama au wa wilaya wa chama husika.

Hivyo, malumbano yanayotokea yanaweza kuchochea hali ya kutokuaminiana kati ya NEC na vyama vya siasa ambavyo, kwa mujibu wa sheria, vyote ni mfano wa watoto wa Tume hiyo.

Tume inapaswa kuwa tayari kuketi meza moja na vyama husika na kuvisikiliza kuliko kuendelea kujibizana kwa kupitia vyombo vya habari, hali inayoendeleza mpasuko kati ya vyama vya siasa na NEC.

NEC wanapaswa kutumia busara zaidi wakati wa kukabiliana na changamoto kama hizo kuliko kujibizana na vyama, hali inayoweza kutafsiriwa kuwa wanatumika kuvikandamiza vyama vingine.

NEC isiasisi ujenzi wa ukuta utakaoitenganisha na vyama vya siasa, ikumbuke kuwa yenyewe ni taasisi inayojitegemea na inategemewa na vyama vyote nchini.

Chadema pamoja na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vilitangaza kutokushiriki uchaguzi huo mdogo wa wabunge unaotarajiwa kufanyika Januari 18, 2018 ikidai kuwa mwenendo wa hali ya kisiasa nchini siyo.

Ni matarajio ya kila Mtanzania kuona NEC ikitekeleza wajibu wake kwa kufuata misingi ya sheria na taratibu zilizopo si ‘kuparurana’ na vyama vya siasa.

Vyama vya siasa vipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama, hivyo ni busara iwapo NEC itakuwa na sintofahamu baina ya chama chochote cha siasa kuwasiliana na Ofisi ya Msajili ili kuondokana na mtifuano usio na tija kwa wapigakura.

NEC ni mali ya kila Mtanzania, hivyo ni matarajio yetu kuona ikisimama kwa ajili ya kila mpiga kura kwa mustakabali wa nchi yetu kwa pamoja.

Mungu Ibariki Tanzania.

By Jamhuri