Na James Mwanamyoto,JamhuriMedia,Dodoma

Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Rushwa Afrika tawi la Tanzania (APNAC) Mhe. Cecilia Pareso (Mb) amesema mtandao wao utashirikiana kikamilifu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa kwani rushwa inakwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Pareso amesema hayo jijini Dodoma wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Rushwa Afrika tawi la Tanzania (APNAC) ili waweze kushirikiana vema na TAKUKURU katika kuitokomeza rushwa nchini.

“Sisi wabunge ambao ni wajumbe wa Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Rushwa Afrika tawi la Tanzania kwa pamoja tunaunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha rushwa inatokomezwa nchini kwa sababu kukiwa na rushwa wananchi hawawezi kupata huduma wanayostahili,” Mhe. Pareso amesisitiza.

Naye, Katibu Mkuu wa Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Rushwa Afrika tawi la Tanzania, Mhe. Vita Kawawa (Mb) amesema semina waliyopatiwa imekuja wakati muafaka kwani itawawezesha kupata elimu ya kutosha ya jinsi ya kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Mhe. Vita Kawawa amesema kuwa, semina waliyopatiwa itakuwa na manufaa kwa waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Rushwa Afrika tawi la Tanzania, kwa sababu wanatoka katika maeneo ambayo fedha nyingi za miradi zimeelekezwa na Serikali, hivyo watatumia elimu waliyoipata kuzuia mianya ya rushwa ambayo inaweza kukwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo wajumbe wa APNAC wakimuunga mkono kupambana na rushwa kwa kushirikiana na TAKUKURU watawezesha fedha za miradi kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Ndejembi ameongeza kuwa, anaamini baada ya wajumbe hao wa Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Rushwa Afrika tawi la Tanzania kupatiwa semina hiyo ya kuwawezesha kupambana na vitendo vya rushwa, watakuwa na ari na nguvu zaidi ya kukemea vitendo vya rushwa katika jamii inayowazunguka ikizingatiwa kwamba, wajumbe hao ni wajumbe wa kamati za fedha katika halmashauri zao.

Akizungumza kuhusu lengo la TAKUKURU kuandaa semina hiyo kwa wajumbe wa APNAC, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni amewaomba wajumbe wa APNAC kusaidia kuwahamasisha waheshimiwa wabunge wengine kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi pindi wanapokutana nao katika mikutano na shughuli mbalimbali za kijamii.

Wajumbe wa Mtandao wa Wabunge wa Kupambana na Rushwa Afrika tawi la Tanzania (APNAC) kupitia Semina hiyo ya siku moja iliyoandaliwa na TAKUKURU walipata fursa ya kupitishwa kwenye mada iliyohusu wajibu wao katika kuzuia vitendo vya rushwa nchini

By Jamhuri