Zoezi la kushusha meli moja ya MV. Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ limefanyikwa vyema kwa asilimia 100 na ujenzi wake umefikia asilimia 82.

Akizungumza Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-Uchukuzi Atupele Mwakibete kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Profesa Makame Mbarawa, wakati wa hafla ya ushushaji wa meli hiyo iliofanyika Bandari ya Mwanza Kusini, jijini Mwanza.

Amesema kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Mel (MSCL), imetakiwa kuendelea kusimamia mradi wa ujenzi wa meli hiyo ili ukamilike ndani ya muda uliopangwa na kuanza kuwahudumia wananchi.

Pia kuhakikisha kuwa inasimamia miradi yote inayotekelezwa na Serikali kama ilivyopangwa na kuleta thamani ya fedha iliyowekezwa.

Pia ametoa rai kwa MSCL kuhakikisha inajipanga kuendelea kuboresha Bandari katika Ziwa Victoria ili meli hiyo iweze kutoa nanga bila shida wakati itakapoanza safari zake pamoja na gati lililopo mkoani Mara.

Mwakibete ameeleza kuwa,serikali imekuwa ikiwekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na MSCL kwa lengo la kuboresha huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya meli.

Amesema kuwa kujengewa kwa meli hiyo kutasaidia kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha safari mpya zitakazosaidia kurahisisha shughuli za kibiashara,kikazi,utalii na safari binafsi kwenye maeneo mengi zaidi ya ilivyo sasa.

“Meli hii itakapo kamilika ndani ya mwaka huu siyo tu kutakuwa na ongezeko la meli bali pia usafiri huu,utakuwa umeboreshwa sana kwa vile meli itakuwa ya kisasa na yenye mwendo kasi mkubwa zaidi ya meli zilizopo,”ameeleza Mwakibete.

Sanjari na hayo Mwakibete ameielekeza Menejimenti ya MSCL kubainisha vijana waliopata utaalamu kupitia mradi huo waweze kutumika kadri ya mahitaji ya kampuni yatakavyojitokeza ili nguvu kazi yenye uzoefu isipotee.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL Erick Hamissi,ameeleza kuwa meli hiyo ikikamilika itahudumia bandari zote Kuu za Ziwa Victoria ikiwemo ya bandari ya Kemondo, Bukoba,Mwanza,Musoma na Portbell na Jinja za nchini Uganda pamoja na Kisumu nchini Kenya.

Hamissi ameeleza kuwa,meli hiyo ya Mv.Mwanza Hapa Kazi Tu,ina uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo na magari madogo 20 hadi kukamilika kwake itagharimu kiasi cha bilioni 109.

“Wakati serikali ya awamu ya sita inapokea mradi huo ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 45 laki mpaka leo inavyoshushwa ndani ya maji imefikia asilimia 82, huku Mkandarasi ameishalipwa asilimia 88 sawa na bilioni 93.8,”ameeleza Hamissi.

Ameeleza kuwa meli hiyo itakuwa na madaraja sita ambayo ni VIP itakayokuwa maalum kwa viongozo wa kitaifa ambapo watakuwa wanakaa watu wawili tu pamoja na viongozi wa kitaifa wa nchi jirani kama watapata kibali cha kusafiri na meli hiyo.

Huku ameeleza kuwa daraja la VIP ambalo litabeba watu mashuhuri sehemu hii itakuwa na watu wanne yaani vyumba vinne, daraja la kwanza litakalokuwa na watu 60, daraja la biashara litakalokuwa na watu 100 daraja la pili litakalokuwa na watu 200.

“Daraja la mwisho kwenye meli hii litakuwa ni la uchumi ambalo litakuwa linabeba abiria 834 na katika daraja hili kutakuwa na hadhi ya kisasa na wananchi watakaa kwa starehe na wataweza kufanya utali,”ameeleza Hamissi.

Ndani ya meli hii pia kutakuwa na buradani,kutakuwa na sehemu ya lift hasa kwa watu wenye changamoto ya kupanda ngazi na wagonjwa, na sehemu ya hospotali (dispensary) na sehemu ya wamama wajawazito

“Tunatarajia meli hii itakuwa inatumia masaa 10 pekee kwenda bandari ya Portbell nchi Uganda lakini pia itaenda Musoma mkoani Mara,” ameeleza Hamissi.

By Jamhuri