Na Daniel Limbe, JamhuriMedia, Chato

Wakati waumini wa dini ya kikristo duniani wakiendelea kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, huko wilayani Chato mkoani Geita kumetokea mauaji ya mwenyekiti wa kitongoji cha Mwabazengi, Kata ya Muungano, Robert Msodock, baada ya kukutwa akiwa na mke wa mtu.

Tukio hilo linadaiwa kusababishwa na wivu wa mapenzi, baada ya mwenye mke aliyefahamika kwa jina la John Mbonge, kumkamata mtuhumiwa akiwa na mke wake jana kwa madai kuwa walikuwa wakielekea nyumba ya kulala wageni kwenye kijiji cha Itale Branchi (Kahumo).

Mashuhuda wa tukio hilo,wanaeleza kuwa marehemu amekuwa akifanya uzinifu na mke wa mtu tangu mwaka 2018 na kwamba kabla ya umauti huo tayari alikuwa ameshafumaniwa mara mbili.

Pamoja na fumanizi hizo,alikuwa akilipa faini ya fedha ikiwa ni adhabu.

Katibu wa ulinzi wa Jadi, (Sungusungu) kijiji cha Itale Stoo, Enos Joseph,amekiri kuwa marehemu amekuwa akifumaniwa mara kwa mara na kwamba fumanizi lililosababisha kifo chake ni la awamu ya tatu.

“Ni kweli marehemu ameshafumaniwa mara mbili na hili tukio ni la tatu…bahati njema baada ya kupewa taarifa za kuwa amefumaniwa jana,mimi na viongozi wenzangu wa sungusungu tulikwenda eneo la tukio kwa ajili ya kumkamata…tulipofika pale tulimkuta amelala chini akiwa hai lakini hali yake ilikuwa mbaya sana…nilimuuliza kama ananijua akajibu ndiyo na kunitaja jina langu la Eno”

“Baada ya kunitaja jina nilimuuliza imekuwaje … akaniambia kutongoza wake za watu ndiyo imenifanya kuwa hivi…nikamuuliza tena simu yako iko wapi akasema John ndiyo kaichukua baada ya kunikatakata na mapanga…baada ya ma meno hayo hakuongea tena tukamchukua na kumkimbiza hospitali ya Wilaya ya Chato kwa matibabu”amesema Joseph.

Amesema wakiwa hospitalini hapo nesi aliowapokea alimpima mgonjwa wao kisha kuwajulisha kuwa ameshafariki baadaye akapelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Mwenyekiti wa kijiji cha Itale Stoo, Njingo Lubinza, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo huku akidai limetokea akiwa safarini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,Saphia Jongo, amekiri kuwepo kwa tukio la mwenyekiti huyo kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kukutwa akiwa amesimama na mke wa mtu, huku akidai hajapewa taarifa za kifo cha majeruhi huyo.

“Nilipewa taarifa za mwenyekiti huyo kujeruhiwa vibaya upande wa paja la kulia,mkono na kichwani kutokana na wivu wa mapenzi na kwamba hali yake ilikuwa mbaya…taarifa za kuwa ameshafariki hizo nilikuwa bado sijatumiwa”amesema Jongo.

Hata hivyo amedai kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo alikimbia baada ya kutenda kosa hilo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.

Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Chato,Madili Sakumi, alipotafutwa kwa njia ya simu,amethibitisha kupokea kwa taarifa hizo.

“Nimepokea taarifa za tukio hilo muda si mrefu kutoka kwa Polisi jina nimelisahau…alikuwa akiniomba tufanye “Postimotam” ili tukabidhi mwili wa marehemu kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi”amesema Sakumi.

By Jamhuri