silhouettes of a heterosexual couple quarreled and turned away from each other and between the pair a red line

NA BASHIR YAKUB

Watu wengi wamekuwa wakijiuliza ikiwa mmoja wa wanandoa aliyesababisha ndoa kuvunjika kama anastahili mgawo wa mali. Mfano, mwanamke katika ndoa anaanzisha chokochoko makusudi ili ndoa ivunjike apate mgawo wa mali ili aendelee na maisha yake. 

Au mwanamume kwa tabia zake mbaya za ulevi au kutokuwa mwaminifu anasababisha ndoa kuyumba hadi kuvunjika kabisa. Je, kwa sababu amesababisha matatizo na ndiye chanzo cha tatizo mpaka ndoa kuvunjika anastahili mgawo wa mali?

Mara nyingi tumeeleza kuhusu ndoa kuvunjika na misingi ya kugawana mali ambayo imewekwa na sheria hususan Sheria ya Ndoa. Kifungu cha 114 cha Sheria ya Ndoa kwa ujumla kinaeleza misingi ya kuzingatia wakati wa kugawana mali ndoa

inapovunjika. 

Lakini kifungu hichohicho, kifungu kidogo cha 2(b) kinaeleza kwa umahususi kuwa kitu kikubwa ambacho kinapaswa kuzingatiwa wakati wa kugawana mali ni mchango wa kila mwanandoa katika kupatikana kwa mali husika. Yaani ni swali la mwanandoa amechangia nini mpaka hii mali imepatikana.

Tafsiri ya mahakama kuhusu mchango wa mwanandoa katika kupatikana mali ni pamoja na mchango wa pesa, mchango wa kazi (nguvu), pia kazi za nyumbani ambazo mara nyingi hufanywa na mwanamke kama kufua, kupika, kulea watoto,

kutunza nyumba – nazo zinahesabika ni mchango katika kupatikana mali ambazo zitachumwa na mwanamume moja kwa moja huko kazini anakoenda.

Hii ni tafsiri katika rufaa namba 9 ya 1983, TLR 32 katika kesi maarufu ya Bi Hawa, ikifuatiwa na utitiri wa tafsiri nyingi kama hizo kutoka Mahakama Kuu na ya Rufaa. Huu ndio msimamo wa sheria na haya tumeyarudia mara nyingi.

Swali kuu la mada ni ikiwa aliyeleta chokochoko mpaka ndoa kuvunjika kama naye anastahili kupata mgawo wa mali, au asipate kabisa kwa kuwa ndiye aliyeleta ugomvi, au apate kidogo. 

Mahakama kupitia kesi ya ROBERT ARANJO v ZENA MWIJUMA (  ) [1985] TZHC 5; (14 March 1985); 1984 TLR 7

(TZHC) itatujibia swali hili. Katika kesi hii mkata rufaa ambaye ni mwanandoa, Robert Aranjo alikata rufaa Mahakama Kuu akiilalamikia Mahakama ya Mwanzo na ya Wilaya kwa kumpatia mke wake robo ya mali kama mgawo wake wakati mwanamke huyohuyo ndiye aliyesababisha ndoa kuvunjika baada ya kuamua kuondoka mwenyewe nyumbani kwa sababu anazozijua yeye.

Kwa hiyo Robert aliamini kuwa mwanamke huyo hastahili mali aliyopewa kwa kuwa yeye ndiye sababu ya kuvunjika kwa ndoa.

Jaji Maina (kama alivyokuwa), alitoa uamuzi kuwa suala la nani amesababisha ndoa kuvunjika halina uhusiano wowote na suala la nani anatakiwa kupata nini. Alisema kuwa katika mambo yanayozingatiwa wakati wa kugawana mali pale ndoa inapovunjika swali la nani amesababisha ndoa ivunjike halina nafasi. 

Alisema kinachozingatiwa na kuangaliwa ni kile kilichoelezwa katika kifungu cha 114 cha Sheria ya Ndoa ambacho ni pamoja na mchango wa mwanandoa katika kupatikana kwa kila mali husika.

Kwa hiyo kwa wale waliotaka kujua kuhusu hatima ya waanzilishi wa chokochoko katika ndoa, basi hili liko hivi. Suala la nani ameanzisha ugomvi haliangaliwi wakati wa kugawana mali. Aidha, suala hili linaweza kuangaliwa katika mazingira mengine, kwa mfano zinapokuwa zinajadiliwa sababu zilizosababisha ndoa kuvunjika, na katika masuala ya fidia kwa mwanandoa, lakini si katika kugawana mali. Kwa hiyo hivi ndivyo ilivyo.

By Jamhuri