Katibu Mtendaji, Baraza la Mitihani la Tanzania anapenda kuwajulisha watu wote wanaotaka kufanya Mtihani wa kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT) mwezi novemba, 2018 kama watahiniwa wa kujitegemea kwamba:

  1. Kipindi cha usajili kwa watahiniwa wa kujitegemea kimeanza tarehe 1 Januari, 2018 kwa ada ya shilingi 50,000/= kwa wanaojisajili CSEE na shilingi 30,000/= kwa wanaojisajili QT na kitaisha tarehe 28 Februari, 2018. Aidha, watakaojisajili kwa kuchelewa kuanzia tarehe 01/03/2018 hadi tarehe 31/03/2018 watalipa shilingi 65,000/= kwa watahiniwa wa kidato cha Nne (CSEE) na shilingi 40,000/= kwa watahiniwa wa mtihani wa Maarifa (QT) ikiwa ni ada ya kawaida pamoja na faini.
  1. Mtahiniwa atakaye jisajili kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2018 ni yule ambaye anarudia Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) au amefanya na kufaulu Mtihani wa Maarifa (QT) katika kipindi kisichozidi miaka mitano (5) iliyopita au mwenye sifa zinazolingana na hizo alizopata kutoka nje ya nchi na kufanyiwa ulinganifu na Baraza la Mitihani la Tanzania.

 

  1. Mtahiniwa atakayejisajili kufanya Mtihani wa Maarifa ni yule ambaye anatafuta sifa ya kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne kama Mtahiniwa wa kujitegemea.

 

  1. Kabla ya kujisajili kwenye mtandao, waombaji wanapaswa kwenda kwenye vituo vya mitihani kuchukua namba rejea (reference number) zinazotolewa bure na kufanya malipo ya ada ya mtihani katika ofisi za Posta pekee.

 

  1. Waombaji wote wanasisitizwa kuhakikisha wanajisajili mapema kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya baraza la Mitihani ya necta.go.tz kwani mfumo wa usajili utafungwa baada ya kipindi cha usajili kumalizika.

Imetolewa na:

KATIBU MTENDAJI

By Jamhuri