Polisi yavunja mkataba na kocha mkuu

KLABU ya Polisi Tanzania imeachana na kocha wake Mrundi, Joslin Sharrif Bipfubusa baada ya miezi mitatu tu tangu ajiunge na timu hiyo Julai 26.

Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Polisi Tanzania kuchapwa 2-0 na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jana Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.

Kwa ujumla mwenendo wa Polisi haukuwa mzuri chini ya Bipfubusa, kwani katika mechi tisa ilizocheza hadi sasa imeambulia pointi tano tu kufuatia kushinda moja na sare mbili, huku nyingine zote sita ikipoteza.