NA Mussa Augustine, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako amewataka Mawakala Binafsi wa Ajira ndani na nje wanapowatafutia Watanzania ajira nje ya nchi wazingatie utu na kwamba wasipofanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuwafutia leseni zao.
Agizo hilo amelitoa Oktoba 23,2023 wakati alipokutana na Wakala binafsi wa huduma za ajira ajili ya Kujadili namna ya kuongeza ufanisi na kutatua changamoto zinazowakabili mawakala hao.
Profesa Ndalichako amesema kuwa mawakala hao wazingatie matakwa ya kisheria katika kuendesha shughuli zao,hivyo wanapaswa kuhakikisha watanzania wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria.
Aidha pia amewataka mawakala hao kutovuka mipaka yao ya kazi ikiwemo kushikilia mishahara ya wafanyakazi waliowatafutia ajira,huku wakiwachukulia nusu ya mishahara,ambapo amesema wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Amesema kuwa Serikali ilisitisha huduma za ajira nje ya nchi mwaka 2018 baada ya serikali kuona mawakala hao walikuwa wanaangalia kipato kuliko utu wa mtanzania.
“ Mawakala mnapowapeleka Watanzania nje ya nchi utu wa mtanzania uthaminiwe, Serikali haipo tayari kuona wananyimwa stahiki zao,hawana mikataba na wakitaka kuondoka hawana uhuru wa kurudi nyumbani,serikali itachukua hatua kwa wakala yeyote atakaebainika”amesisitiza Profesa Ndalichako Nakuongeza kuwa “Nawasihi mawakala wote kuzingatia matakwa ya kisheria katika kuendesha shughuli zenu na wale wachache wanaokiuka misingi ya kisheria watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufuta leseni.
Ameongeza kuwa wapo mawakala wachache wanaofanya shughuli hapa nchini ambao hawazingatii sheria ikiwemo kujihusisha na mahusiano ya kiajira na wafanyakazi wanaotakiwa kuwaunganisha na waajiri wanashindwa kuwapatia wafanyakazi wao mikataba ya ajira na kutowachangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Profesa Ndalichako alisema vitendo hivyo ni ukiukwaji wa sheria za kazi pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Amesema Serikali imeruhusu mawakala binafsi kuunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kufanyika ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 takribani mawakala 83 walisajiliwa kati ya hao 56 wamehuisha leseni zao kwa mwaka 2023/24.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Cyprian Luhemeja amewataka mawakala hao kushirikiana na serikali kumaliza changamoto ya ajira nchi.
“Naamini leo tutajadiliana jinsi ya kuongeza ubunifu na ufanisi katika kuboresha na kumaliza changamoto ya ajira nchini kwasababu Tanzania tumechelewa sana kupeleka watanzania nje ya nchi hivyo serikali inawaunga lakini kwa kufuata utaratibu mzuri wa kuwapeleka watanzania nje na utaratibu uwe wa leseni,” alisema Luhemeja.
Mwakilishi wa mawakala binafsi wa Ajira ndani na nje ya nchi ,Bona Manyema alisema anaishukuru Serikali kwa kuwawekea mazingira wezeshi na wameahidi kufuata tararibu hivyo atakayeenda tofauti na hayo atachukuliwa hatua za sheria.