Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam

Raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ameishukuru Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa huduma bora za matibabu ya saratani zinazotolewa kwa mama yake anayepata matibabu katika taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Patrick Yuma ambaye mama yake anatokea Kinshasa nchini DRC ameeleza kuridhishwa na namna walivyopokelewa pamoja na huduma wanazopata tangu walipofika ORCI kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza na mwandishi wa Habari hii jijini Dar es Salaam, Yuma alisema walifika ORCI mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu baada ya mama yake kufanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya CMCK iliyopo jijini Bujumbura nchini Burundi.

Alisema baada ya uchunguzi huo walielekezwa kufika ORCI kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya saratani hususan matibabu ya mionzi na familia iliamua kuchagua Tanzania miongoni mwa maeneo waliyokuwa wamepewa kama machaguo ya kupata matibabu.

“Tumefika hapa mwanzoni mwa mwezi wa nane na mama yangu anaendelea vizuri na matibabu na anatarajia kumaliza matibabu yake wiki chache zijazo jambo ambalo limetupa matumaini katika safari yake ya matibabu. Huduma ni nzuri sana na wametupokea vizuri,” alisema Yuma.

Alisema awali familia ilikuwa na chaguo la kwenda Zambia au Tanzania kwa ajili ya matibabu lakini waliamua kumleta mama yake ORCI kutokana na ushauri walioupata baada ya uchunguzi wa awali kufanyika Bujumbura.

Aidha Parick aliwataka wagonjwa wa saratani kutokata tamaa wala kukaa na wagonjwa nyumbani bila kuwapeleka kupata huduma za kitaalamu huku akisisitiza kuwa saratani inaweza kutibiwa na wagonjwa wakapona kulingana na aina na hatua ya ugonjwa.

“Watu wasikae na wagonjwa nyumbani. Wawapeleke Hospitali wakatibiwe. Na wafahamu kuwa wanakuja hospitali kutibiwa na watapona. Mimi nimeona hapa watu wengi wanakuja kutibiwa, wanapata huduma nzuri na wanapona,” alisema Yuma.

Alisema uzoefu wao wa kupata matibabu katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) umewapa matumaini ya kuona mgonjwa anatibiwa na kupona na kuwataka wagonjwa wengine kutumia huduma za kitaalamu badala ya kuchelewa kutafuta matibabu.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha kliniki ya bima, wagonjwa maalumu na wanaotoka nje ya nchi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Caroline Swai alisema taasisi hiyo imeendelea kupokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani.

Dkt. Caroline alisema wagonjwa hao wanatoka katika nchi mbalimbali zinazopaka na Tanzania na zile ambazo hazipakani na Tanzania zikiwemo za Zambia, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Kenya, Msumbiji, Thailand, Malawi, Samoa ya Marekani na Afrika Kusini.

“Kupokea wagonjwa kutoka nje ya Tanzania kunaonesha kuwa ORCI imeendelea kuwa miongoni mwa taasisi zinazotoa huduma za kibingwa za saratani zinazowafikia wagonjwa kutoka ndani na nje ya nchi”, alisema Caroline.

Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) inaendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani kwa Watanzania na wagonjwa kutoka nchi mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua upatikanaji wa huduma za kibingwa za saratani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.