Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitakubali urasimu ama vikwazo kukwamisha shughuli za wawekezaji, akisisitiza kuwa mkoa upo nyuma kusimamia vikwazo na kero za wawekezaji.
Nyongo ameyasema hayo oktoba 8,2026 wakati alipotembelea migodi ya Kinywe (Graphite), ikiwemo kiwanda cha AAMS Mining DMCC Graphite Project na Kusini Gateway Co. Ltd., katika Kata ya Mkange, Chalinze, kabla ya kuzungumza na wananchi wa Msata.
Amesema miongoni mwa changamoto zinazoukabili mradi wa AAMS ni suala la kikodi, ambalo limewafanya baadhi ya wawekezaji kusita kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya uwekezaji, hali iliyosababisha wafanyakazi 250 kuondoka kutokana na kusimama kwa shughuli za mradi.
“Tumepata changamoto inayomkabili mwekezaji AAMS, wenzake walioleta fedha wameingiwa na hofu ya kuendelea kutoa fedha kutokana na suala la kikodi, hali hiyo imesababisha watumishi 250 kuondoka kwa sababu ya taratibu za kikodi ambazo zimefanya mwekezaji ashindwe kuendelea na uwekezaji,” ameeleza Nyongo.
Aidha, Nyongo amesema atawasiliana na Wizara ya Madini ili kushughulikia na kusimamia masuala ya leseni na kikodi yanayohusisha shughuli za uchimbaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amesema changamoto hiyo imeanza kuchukuliwa hatua, ikiwemo kuundwa kwa tume ya wilaya kwa ajili ya kufuatilia na kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Mwekezaji, Jumbe Nungu, amefafanua wamejipanga kuwekeza Dola milioni 100, sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 264, katika mradi huo, ambao ulianza mwaka 2024 na wanatarajia kuanza uzalishaji kabla ya mwaka 2027.







