Rais wangu utatukuzwa kwa mema yako (2)

Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, mjukuu wako, yaani binti yangu amejiunga Chuo Kikuu Mlimani kwa mwaka wa kwanza akichukua Sayansi na Teknolojia.

Amesoma  kidato cha tano na cha sita Ifakara High School – shule ya Serikali. Amenyimwa mkopo eti zamani akiwa madarasa ya chini aliwahi kusoma shule ya kulipia. Mungu ailaze mahali pema peponi, roho ya marehemu aliyemlipia binti yangu wakati ule!

Baba Mwadhama, mpaka nafika umri huu, kila nilipokabiliwa na magumu kama haya, nilipomlilia Muumba wangu kuwa nimefika mwisho, hajawahi kuniacha! Basi, nimemthibitishia binti yangu kuwa Mungu ni mwema utasoma mpaka mwisho! Baba Mwadhama binti yangu tumwachie Mwenyezi Mungu! Lakini mwambie baba awatazame watoto wa masikini waliotapakaa nchi nzima ambao wamekosa mikopo ya elimu ya juu katika awamu hii ya tano.

Nanyi wanangu watoto wa masikini mliokosa mikopo msikate tamaa, Mungu ni mwema. Msimtangulize Mungu mbele, mwacheni akae katika vifua vyenu naye hatawaacha! Maombi ya wenye haki Mungu anasikia! Wapandao kwa machozi watavuna kwa shangwe! Lieni, ombolezeni japo kwa siri Mungu atawasikia!

Baba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, jinsi paa anavyotamani vijito vya maji, ndivyo roho yangu inavyotamani kuuona uso wa Muumba wangu! Natambua bado kidogo nitakuwapo na bado kidogo tena sitakuwapo kwa kuwa nyakati za kwenda kuungana na marehemu wazazi wangu unazidi kuwa dhahiri.

Kumbuka Mwadhama tulikotoka ni mbali. Ukiwa juu nikiwa chini, lakini shule yetu ya maadili mema ilikuwa ni moja – Kaengesa Seminari. Ukitazama juu jua letu sasa linaelekea kuzama! Kwanini katika uzee huu kuanza kuhangaika na mambo ya kidunia? Busara wakati mwingine ni kuwa kimya!

Baba Mwadhama, nimeitumikia nchi yangu kwa uadilifu mkubwa kwa miaka 20 na sasa nimestaafu. Baba ananilipa pensheni shilingi elfu 50 kwa mwezi! Namwachia Mungu! Lakini Baba Mwadhama mimi niache na Mungu wangu! Kwa kuwa unasikiwa na baba, mwambie awahurumie baba zake, kaka zake, dada zake na mama wale wazee wastaafu ambao mpaka leo anawalipa pensheni ya shilingi elfu 50 kwa mwezi. Amesema siku zote pesa zipo! Mkumbushe kuwa Bunge liliamuru waongezewe shilingi elfu 50 wakati anaingia madarakani ili angalau kwa mwezi wapate laki moja.

Miaka minne amemaliza amekuwa kama hawaoni. Wazee wanazidi kupukutika! Mwambie sasa wamebaki wachache awalipe kabla hawajamalizika wote! Baraka na laana vyote hutoka kwa wazee! Kwa uadilifu wao ndiyo walioifikisha nchi hii hapa na sasa watu wanajidai. Awalipe ili Mwenyezi Mungu amhesabie katika fungu jema.

Dunia ni watu! Wafanyakazi wanalia! Mwaka wa nne mfululizo hawajawahi kuiona nyongeza yao.  Wanasadikishwa wamtangulize Mungu mbele. Wakulima wa korosho Mungu awape moyo wa subra wakati huu ambao wakulima wanalia! Kwa mahubiri yako yale ya kusifu makubwa, waumini wakutofautisheje baba Mwadhama na yule aliyesema Baba amefanya miujiza kuliko aliyofanya Yesu kwa wana wa Israel? Ole wetu sisi wana wa kizazi hiki ambao tunaona damu ya mwanadamu na damu ya mnyama kuwa zote ni damu sawa! Wana heri watu wale wajiepushayo  na unafiki wa kuvaa kanzu nyeupe sana wasizoziamini wakitaka kuaminisha wenye imani yao kuwa wanafanya ibada.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuja Mbeya mwanzoni mwa Uhuru alikataza bunduki kuingia kanisani akisema mlinzi wake wa kweli yu hai! Leo watu wanaabudu wakiwa na bunduki mkononi katika nyumba za ibada. Kumbe nao wamejaa hofu!

Baba Mwadhama, ulipolazwa Muhimbili tulikuombea. Uliporuhusiwa kutoka siku hiyo hiyo masikini kutoka Mwanza walikuwa wanaukabidhi mwili wa mpendwa wao kwa uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ili azikwe pamoja na mingine wanayozika baada yakushindwa kulipa gharama za kukomboa maiti! Mwadhama ni mara ngapi umezitembelea zahanati za kule Mwazye utokako? Masikini wanaandikiwa dawa za kununua bila kujali kama wana uwezo au la! Ni kweli Yesu aliahidi, majira ya jioni atarudi, lakini naamini hatatukuta! Ningemshitakia pensheni ya wazee mbele yao!

Baba Mwadhama, Muumba wangu alinijalia kuufikia mlima ule ambao Yesu alijaribiwa. Akiwa juu Yesu alionyeshwa fahari yote ya dunia. Akaambiwa na shetani, ukinisujudia nitakupa yote haya! Yesu alikataa akamwambia ondoka kwangu ewe shetani. Imeandikwa utamsujudia Bwana Mungu wako peke yake!

Leo Kardinali Pengo kuahidiwa mtaa tu kupewa jina lake, na hata haujulikani kama mtaa huo utakuwa Uwanja wa Fisi au Manzese kwa Mfuga Mbwa, anatoa maneno ya kusifia yanayomsukuma Mtumishi wa Mungu Baba Askofu Munga aseme ametoa kauli zinazoweka utukufu kwa wanadamu na si kwa Mungu. Waamini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Wakristu wengine wenye mapenzi mema wanajiuliza, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, angekuwa ndiye Yesu, badala ya kuahidiwa ka-mtaa, akaahidiwa fahari yote ya dunia kama alivyoahidiwa Yesu, hivi kweli leo kuna mtu angekombolewa? Hakika huyu, angeusaliti Msalaba! Yawezekana Mwenyezi Mungu hakutaka niwe padri kwa kuhofia kuja kulichafua Kanisa lake kama hivi! Basi, kama hivyo ndivyo, jina la Bwana lihimidiwe!