Serikali imejipanga kuja na mpango wa ufugaji nyuki ujulikanao kama Manzuki ambapo nyuki watakuwa wanafugwa katika eneo maalum bila kuathiri uhifadhi.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Uyovu Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita.

Amefafanua kuwa kupitia mpango huo wananchi wataweza kufuga nyuki na kupata faida bila kuhama kuhama.

Kuhusu wananchi wanaofuga nyuki katika Hifadhi ya Kigosi, amesema kuwa Serikali imeruhusu wananchi kuendelea na shughuli za ufugaji nyuki wakati inatafuta eneo mbadala la kuwahamishia wafugaji hao.

“Tamko la Serikali ni kwamba shughuli za ufugaji nyuki zitaendelea hadi pale tutakapotoa mbadala wa wapi mpeleke mizinga yenu.” Mhe. Masanja amesisitiza.

Aidha, amewataka wananchi kukitumia ipasavyo Kiwanda cha kuchakata asali kilichopo katika eneo hilo ili waweze kuuza asali kwa faida.

Amewataka wananchi kutunza mazingira na kuacha kukata miti hovyo ili kuendelea kufaidika na mazao yatokanayo na nyuki.

Awali, Waziri wa Madini na mbunge wa jimbo la Bukombe Mhe.Dkt.Doto Biteko amesema, Mhe.Rais Samia anataka kuona kero za wananchi wakiwemo wa Uyovu zinatatuliwa na ndiyo maana Mhe.Naibu Waziri amefika, hivyo kuwasihi wananchi kuwa wahifadhi kwa kuilinda misitu ya Bukombe isiharibiwe.

Naibu Waziri Mary Masanja anaendelea na ziara yake katika Kanda ya Ziwa kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazoikabili Sekta ya Maliasili na Utalii.

By Jamhuri