SERIKALI imeanzisha mpango kabambe wa kutumia tafiti zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika na wataalamu wa ndani ili kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii.

Akizungumza katika Uzinduzi wa Kigoda cha Utafiti cha Oliver Tambo (Oliver Tambo Research Chair for Viral Epidemics) uliofanyika katika Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga amesema katika kutekeleza mpango huo Serikali imetenga Shilingi bilioni 9 katika mwaka wa fedha 2022/2023 ili kuchochea maendeleo na matumizi ya tafiti katika nyanja ya Sayansi, Ubunifu na Teknolojia .

Naibu Waziri Kipanga amesema bajeti hiyo ya kufanya na kuendeleza tafiti nchini imeongezeka kutoka bilioni 3 mwaka wa fedha uliopita ikiwa ni hatua ya Serikali kuhakikisha matatizo yaliyopo kwenye jamii yanapatiwa ufumbuzi kwa njia za kitaalamu.

“Wakati tunapata uhuru ujinga ulikuwa ni moja ya maadui, hatuwezi kuondoa ujinga bila kufanya tafiti. Maendeleo yatapatikana kama tutaondoa ujinga kwanza,” amefafanua Mhe. Kipanga.

Kuhusu tafiti nyingi kutotumika na kufungiwa kwenye makabati, Mhe. Kipanga amesema kwamba utayari wa Serikali kuongeza bajeti ni ishara ya kwamba nchi imeamua kwamba tafiti hizo zinakwenda kutumika kutatua changamoto.

Naibu Waziri Kipanga amesema kwamba mpango huo utatekelezwa kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambayo itakuwa inaratibu tafiti zote ili kutoa kwenye maaandishi na kuziingiza kwenye matumizi.

“Kupitia tafiti hizi tunakwenda kutatua changamoto zilizopo, lengo kubwa sio tafiti hizi kubaki tu kwenye makaratasi, ” amesema Kipanga.

Kipanga amezitaka taasisi zote zinazofanya tafiti nchini kushirikiana na COSTECH ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinatoa majibu katika changamoto zinazoikabili jamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kigoda cha Utafiti cha Oliver R.Tambo nchini, Prof. Gerald Misinzo kutoka Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) amebainisha kwamba lengo kuu la uanzishwaji wa kigoda hicho ni kupambana na magonjwa ya kuambukiza ili kuboresha afya ya binadamu na mifugo kupitia tafiti kutoka taasisi za elimu na wanazuoni wake.

Prof. Misinzo amebainisha kwamba Kigoda cha Tafiti cha Oliver R.Tambo inashirikiana na SACIDS Foundation katika mpango wa One Health ulioanzishwa mwaka 2008 na vyuo mbalimbali katika nchi tano za Wanachama wa SADC ikiongozwa na SUA.

Mwenyekiti huyo amesema uanzishwaji wa Kigoda hicho cha tafiti utawezesha kuleta mabadiliko chanya katika jamii ili kutimiza mpango mkakati wa Chuo cha Sokoine cha Kilimo kwa mwaka 2022, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2025 na Ajenda ya Umoja wa Africa 2063 (Africa we want).

By Jamhuri