TANZANIA na Marekani zimedhamiria kuongeza kiwango cha  biashara baina ya nchi hizo kutoka kiwango cha  Dola milioni 460  zikizofikiwa kuanzia mwaka 2016 hadi 2023.

Balozi wa Marekani nchini , Michael Battle amesema hayo leo Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya biashara yatakayolenga kubaini ukuaji wa biashara pamoja na kutafuta suluhu ya  vikwazo vinavyokwamisha ongezeko la biashara baina ya nchi hizo.

Amesema ushirikiano wa biashara baina ya nchi hizo itasaidia kuongeza ufanyaji biashara baina ya nchi hizo pamoja na kuzifikia fursa mbalimbali zilizopo.

“Marekani ina matumaini makubwa ya kufanya biashara na Tanzania na tunaamini majadiliano yaliyoanza yataweka bayana namna bora ya ufanyaji biashara baina ya nchi hizi,” alisema na kuongeza kuwa zipo fursa za kushirikiana baina ya nchi hizo na kukuza.

Amesema Marekani inaiamini Tanzania na kupitia hatua ya majadiliano hayo imedhamiria kukuza kiwango cha ufanyaji biashara haswa kwa kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya watu wanaofikia milioni 60.

SOMA: https://habarileo.co.tz/tanzania-marekani-kushirikiana-kibiashara/

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk Hashili  Abdallah amesema majadiliano hayo yatajikita katika maeneo manne ikiwemo uchumi wa kidigitali, namna ya kufikia masoko na maboresho ya  kanuni za udhibiti naazingira ya kibiashara na ziara ya maonesho ya biashara.

Amesema kwa majadiliano hayo,Wataalam wa nchi hizo mbili  watajadili namna ya kufikia masoko kupitia mifumo yenye uwazi, kutumia teknolojia ya kidijitali kuleta mageuzi  na ukuaji wa uchumi,.

Kadhalika amesema majadiliano yatashugulikia vyanzo vikuu zinavyoathiri utendaji wa makampuni na kukuza mawasiliano na mahusiano ya moja kwa moja kati ya wafanyabiashara wa marekani na Tanzania

Amesema majadiliano hayo yalitokana na makubaliano yaliyosainiwa Oktoba mwaka Jana baina ya  Waziri wa Biashara wa Marekani na Tanzania kwa lengo la kukuza na kupanua mahusiano ya kibiashara kati ya Marekani na Tanzania.

“Majadiliano hayo yana tafsiri kwa vitendo maono ya Rais  Samia Suluhu Hassan katika falsafa ya kufungua nchi kibiashara,” amesema Abdallah na kuongeza kuwa wadau wa biashara wamekutana Ili kuchambua maeneo hayo.