Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na ushauri wa lishe bora kwa wahandisi kutoka nchi za Afrika walioudhuria mkutano wa 30 wa wahandisi washauri Afrika (FIDIC Africa) Huduma hiyo inatolewa kwa siku mbili katika viwanja vya ukumbi wa kimataifa wa mwalimu Julius Nyerere International Convention Center (JNICC) vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia huduma hiyo daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli George alisema JKCI imeona umuhimu wa kuwasogezea wahandisi huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo karibu kuwapa nafasi ya kuchunguza afya zao.

“Waandisi muda mwingi wanakuwa katika maeneo yao ya kazi (site) na kukosa nafasi ya kufika Hosptitali kwaajili ya kuchunguza afya hivyo kupitia mkutano huu tunawapa nafasi ya kupima afya lakini pia tunawapa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo”, alisema Samweli

Katika kutoa elimu ya mfumo bora wa maisha Dkt. Samweli aliwataka wahandishi kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara na kuijua miili yao kwani magonjwa ya moyo wakati mwingine humtokea mtu bila ya kuonyesha dalili.

Kwa upande wake Mhandisi kutoka Tanroad Magdalena Evance aliwashukuru wataalamu wa afya kutoka JKCI kwa kumfanyia uchunguzi wa afya kwani hajawahi kuchunguza afya yake kama hana changamoto yoyote ya ugonjwa.

“Leo nimejifunza kitu kikubwa sana katika maisha yangu, natakiwa kuchunguza afya yangu kila ninapopata nafasi na nisisubiri hadi niumwe kwasababu tumeambiwa magonjwa yasiyoambukiza wakati mwingine hayana dalili”, alisema Magdalena

Magdalena alisema baada ya kupima amepata ushauri wa namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza elimu ambayo ataizingatia kwani kinga ni bora kuliko tiba.