Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),imewashauri watendaji wake kuacha kutumia mabavu katika ukusanyaji kodi kwa wafanyabiashara badala yake itumie elimu ya kuwahamaisha ili kodi ilipwe bila shuruti.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam katika kikao kazi leo Novemba 15,2022, Mwenyekiti wa bodi ya TRA, Uledi Mussa, amesema kuwa hakuna sababu ya kukusanya kodi kwa mabavu badala yake watumishi wafanye mazungumzo kwa wenye malimbikizo.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo akizungumza wakati wa kikao kazi na wahariri leo Novemba 15,2022 jijini Dar es Salaam.Katikati ni Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Uledi Mussa akimsikiliza na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw.Deodatus Balile.

“Hakuna sababu ya kutumia nguvu katika kukusanya kodi ni vyema watumishi wakakaa pamoja na wahusika na kujadiliana namna ya kulipa madeni bila ya kuathiri shughuli zao za biashara,” amesema mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa TRA katika mwezi Septemba mwaka huu imekusanya takribani trilioni 2.3 ikilinganishwa na lengo la shilingi trilioni 2.2 ambapo makusanyo hayo yanaonyesha kuwa na ufanisi mkubwa wa asilimia 100.5 ya lengo lililowekwa na mamlaka hiyo.

Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Uledi Mussa akizungumza na wahariri wa habari kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya shukrani kwa mlipakodi

“Hii ni dalili nzuri sana ukusanyaji mapato licha ya nchi kuingia kwenye changamoto mbalimbali ikiwemo ya ugonjwa Covid-19, vita ya Urusi na Ukraine ambayo imeathiri uchumi wa dunia ikiwemo Tanzania.

“Pamoja na mazingira hayo taifa limeendelea ukusanyaji mapato kwa kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na wafanyabiashara wameendelea kulipa kodi bila shuruti,’ amesema mwenyekiti huyo.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwenzi Julai hadi Septemba mwaka huu imekusanya jumla ya shilingi trilioni 6 makusanyo hayo ambayo ni sawa na ufanisi wa asilimia 99.1 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 6.1.

Ameongeza kuwa hii ni kutokana na juhudi za utoaji elimu kupitia vyombo vya habariambapo mamlaka hiyo imefanikiwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi hatimaye kukusanya mapato ya serikali jumla ya shilingi Trilioni 6 katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu.

“Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la asilimia 14.6 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha uliopita kwani mwaka huu tulijiwekea malengo makubwa zaidi ya kukusanya mapato ya serikali ikilinganishwa na mwaka uliopita,” amesema.

Ameongeza katika kuadhimisha Wiki ya Mlipa Kodi,Novemba 17, mwaka huu TRA inatarajia kuwatambua walipa kodi bora ikiwa ni hatua ya kuthamini mchango wao kwani pia wamekuwa ni chimbuko la mafanikio katika makusanyo ya kodi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile akizungumza wakati wa kikao kazi kuhusu wiki ya Shukurani kwa mlipakodi kilichofanyika leo Novemba 15,2022 jijini Dar es Salaam.Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayomb na katikati ni Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Uledi Mussa

Hata hivyo katika kikao kazi hichi baadhi ya wahariri walielezea kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazowakumba wafanyabiashara na kuwa kero kwao na hata kukwamisha zoezi la ulipaji kodi kwa hiari ikiwemo utozwaji wa ushuru mkubwa kwenye magari bandarini.

Pia walieleza kuwepo kwa kero ya gharama za ununuzi wa mashine za EFDs ambapo wameshauri mashine hizo zigawiwe bure na TRA ili kazi yao iwe kukusanya kodi tu.

Naye mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema kuwa kuna kero wanayokabiliana nayo vyombo vya habari ya utozwaji wa faini ya kutotumia mashine EFDs katika uuzaji magazeti.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukitozwa faini ya kutotumia mashine katika uuzaji magazeti, mwenyekiti embu fikiria wauza magazeti kwenye barabara wanavyokimbizana na wateja, kisha huyo huyo muuza magazeti ashike mashine za EFDs za kila gazeti hii ili mteha anaponunua amkatie risiti hii ni ngumu na haiwezekani,haiwezekani,haiwezekani popote,” amesema Balile.

By Jamhuri