UBINAFSISHAJI WA TTCL MPAKA KUWA AIRTEL ULIKUWA NA UTATA

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 11 Januari, 2018 amewasilisha taarifa ya kamati aliyoiunda kuchunguza umiliki wa kampuni ya simu Airtel kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyeagiza kufanyika kwa uchunguzi huo tarehe 20 Desemba, 2017.
Baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, Dkt. Mpango amesema Serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.
Kufuatia ukiukwaji huo Dkt. Mpango amesema Serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za kampuni ya Airtel imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa ili nchi iweze kupata haki yake.
“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya hovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao” amesema Dkt. Mpango.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amepokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa tarehe 25 Novemba, 2017 wakati wa ufunguzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (Mloganzila) kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
Baadhi ya maagizo hayo ni kupunguza baadhi ya idara na madaktari katika hospitali ya Taifa Muhimbili na kuhamishia Mloganzila na hospitali za mikoa kuhamishwa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mhe. Ummy Mwalimu amewasilisha taarifa hiyo akiwa ameongozana na viongozi wakuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKHI), Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (MUHAS).
Katika hatua nyingine, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi amekamilisha kanuni za sheria ya madini namba 7 ya mwaka 2017 na kuwasilisha vitabu vya kanuni hizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi.
Akiwa na Naibu Mawaziri wa Madini Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo na Mhe. Doto Mashaka Biteko, Prof. Kabudi amesema kanuni hizo zimekamilika siku moja kabla ya tarehe ya mwisho iliyotolewa na Mhe. Rais Magufuli na kubainisha kuwa sasa sheria inaweza kuanza kutumika.
Kwa upande wao Naibu Mawaziri wa Madini wamewataka Watanzania na wadau wote wa sekta ya madini kushirikiana na Serikali kutekeleza sheria hiyo na wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa msukumo wa kukamilishwa kwa kanuni hizo.