Home Kitaifa NAIBU WAZIRI KWANDIKWA AWATAKA TEMESA KUPELEKA KIVUKO LINDI

NAIBU WAZIRI KWANDIKWA AWATAKA TEMESA KUPELEKA KIVUKO LINDI

by Jamhuri
 Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandika, kuhusu hali ya miundombinu ya barabara, madaraja, vivuko, pamoja na viwanja vya ndege katika mkoa huo. Naibu Waziri huyo yupo katika ziara ya kikazi ya siku 3 mkoani humo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa akizungumza na uongozi wa mkoa wa Lindi katika kikao kazi, kuhusu umuhimu wa wataalamu wote kushirikiana katika masuala ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika mkoa huo. Kulia ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Lindi, Mhandisi Isaack Mwanawima akisikiliza.
 Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoa wa Lindi, Mhandisi Grayson Maleko akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, kuhusu ujenzi wa maegesho ya kivuko kitakachotoa huduma kati ya Lindi Mjini na Kitunda, alipokuwa akikagua ujenzi wake mkoani humo.
 Muonekano wa ujenzi wa maegesho ya kivuko kitakachotoa huduma kati ya Lindi Mjini na Kitunda, ambapo mkataba wa kukikokota Kivuko hiko kutoka Pangani mkoani Tanga kuja Lindi upo katika hatua za mwisho.
 Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Lindi,, Hamida Abdallah akimshukuru Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa kufika mkoani hapo kwa ajili ya kutazama hali ya miundombinu ya barabara, madaraja, vivuko na viwanja vya ndege.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, na Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Lindi, Mhe. Hamida Abdallah, wakikagua ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari ya Lindi inayojegwa na SUMA JKT chini ya uangalizi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), katika ziara ya kikazi mkoani humo.
 
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ameuagiza Uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) makao makuu kusaini haraka mkataba kwa mkandarasi atakayebeba kivuko kipya  kutoka eneo kinapotengenezwa wilayani Pangani mkoani Tanga hadi mkoani Lindi.
Akizungumza mara baada ya kukagua maegesho ya kivuko hicho ambacho kinatarajiwa kutoa huduma za usafiri kutoka Lindi Mjini – Kitunda mkoani humo, Naibu Waziri huyo amewahakikishia wananchi kutegemea kupata huduma nzuri za usafiri kwani ujenzi wa kivuko na  maegesho  yake  kwa sasa umefika katika hatua nzuri.
“Naagiza Mamlaka husika kusaini haraka mkataba kwa mkandarasi atakayebeba kivuko hiki kutoka Tanga hadi hapa ili wananchi waone kwamba kivuko kimefika na kipo tayari kwa ajili ya kutoa huduma”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameridhishwa na ujenzi wa maegesho hayo ambayo kwa sasa ujenzi wake umebakia asilimia 10 na hivyo kutarajiwa kukamilika muda wowote.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa, ametembelea na kukagua uwanja wa ndege wa Lindi ambapo amesema Serikali inaendelea na mpango wake wa kuboresha viwanja vya ndege nchini ili kuimarisha huduma katika usafiri wa anga.
Amefafanua kuwa Serikali kupitia mwaka wa fedha 2018/19 licha ya kuwa na mpango wa kuboresha uwanja huo pia itaboresha Uwanja wa ndege wa Kilwa Masoko lengo ni kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa TEMESA mkoani Lindi, Mhandisi Greyson Maleko, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kujipanga katika kuhakikisha wananchi wa Lindi wanapata huduma bora za kivuko.
Naye, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani humo Mheshimiwa Hamida Abdallah, ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusogeza maendeleo kwa wananchi na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Naibu Waziri Kwandikwa amemaliza ziara ya kikazi ya siku Tatu mkoani humo ambapo ametembelea na kukagua Miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake ili kujionea maendeleo na changamoto zake.

You may also like