Sasa mkulima au mfanyabiashara akitaka kuuza au kununua muhogo, ni lazima aelimishwe juu ya masharti hayo ya mkataba. Mwenye dhamana ya kutoa elimu hiyo ni nani?

Kwa maoni yangu ni Wizara ya Kilimo ambayo ndio imeingia mkataba na Mamlaka za China, mkataba huo uliosainiwa una kipengele kimoja kinachosema mtu au kampuni yoyote yenye nia ya kuuza muhogo kwenye soko la China ni lazima isajiliwe na Wizara ya Kilimo.

Ikishasajiliwa itawasilisha majina ya makampuni au watu hao kwa Mamlaka za China, kwa lugha nyingine huwezi kuibuka kutoka kusikojulikana na ukapeleka muhogo mkavu China, kama jina la kampuni yako halijawasilishwa kwenye mamlaka za kule.

Ni kweli kwamba hata wanunuzi wa muhogo kule China, wanachofanya ni kwenda kwenye mamlaka ya kwao inaitwa AQSIQ wanaulizia wapewe orodha ya wauzaji muhogo waliosajilia, wakikuta hakuna aliyepo, ndio wengi wao wameishia kuja Ubalozini kwetu kuulizia.

Kwa mfano tumeshafikiwa na Shirika moja la Umma hapa China linaloitwa SINOLIGHT mahitaji yao ni kununua tani laki tatu kila mwezi. Kwa kuanzia wapo tayari kununua tani laki moja kila mwezi.

Taarifa zao zishawasilishwa kwa mamlaka zinazohusika, wanachosubiria ni jibu na mwongozo wa namna ya kuendelea. Makampuni mengine pia yameendelea kuulizia pia.

Nimalizie kwa kuelezea kwanini kuna nia kubwa ya China kununua muhogo Tanzania. Sababu kubwa zinazosukuma nia hiyo zipo mbili; China hivi sasa inakabiliwa na changamoto kubwa sana ya uchafuzi wa mazingira kwasababu ya viwanda na matumizi ya makaa ya mawe kuzalisha joto wakati wa baridi.

Serikali nchini China imeamua kuchukua hatua kadhaa kukabiliana na changamoto hiyo. Hatua mojawapo waliyopitisha ni kupunguza matumizi ya fossil fuel kwa asilimia 20 na badala yake watahamia kwenye mafuta yatokanayo na mimea (biofuel).

Muhogo una wanga ambao ni moja ya njia watakazotumia kuzalisha biofuel. Hiyo ina maana kwamba mahitaji ya muhogo  kwa matumizi hayo itaongezeka mbali na mahitaji ya kawaida ya muhogo kwa matumizi ya viwandani na chakula.

Sababu ya pili ni msambazaji wa muhogo nchini China ni Thailand na Vietnam na baadhi ya nchi za Kusini mwa Bara la Asia. Nchi zote hizo kilimo chake cha mihogo ni msimu mmoja na wanapokuwa na msimu wa mvua nchi zote hizo hazizalishi muhogo jambo linalo tengeneza uhaba katika kipindi fulani.

Hali hiyo imesababisha China kutafuta wasambazaji wengine ambao wana misimu tofauti na zile nchi za Kusini mwa Bara la Asia  ili wapate uhakika wa bidhaa hiyo katika kipindi chote cha mwaka.

Nigeria na Ghana ndio nchi za kwanza kupewa fursa hiyo. Kwa bahati nzuri au mbaya, kutokana na mahitaji makubwa ya muhogo kule Nigeria, ambao ndicho chakula chao kikuu, ukiongeza na umbali kutoka Nigeria hadi China, wakulima na wafanyabiashara wa Nigeria hawajalichangamkia soko la China na badala yake wakajielekeza kwenye soko la ndani ya Nigeria.

Ndio sababu ya China kuangalia njia nyingine na Tanzania ikafunguliwa hilo soko, jambo moja lipo wazi kabisa biashara ya muhogo mkavu ina faida kama utaifanya kwa kuwa na mzigo mkubwa na inaleta maana kama uzalishaji ni mkubwa.

Kama kwa hekta moja unaweza kuzalisha tani 12 na zaidi, faida ipo. Lakini kama unazalisha tani 3-4 kwa hekta inaweza isiwe faida katika biashara ya kusafirisha. Sasa namna gani mtu unaweza kuongeza uzalishaji, taasisi za utafiti kama zile za Naliendele zipo na zina uwezo mkubwa tu wa kusaidia kwa hilo.

Vilevile mbali na taasisi zetu, upo uwezekano pia wa kupata msaada wa kitaalamu kutoka Thailand ambao wamepiga hatua kubwa katika kilimo cha muhogo. Nimeongea na Balozi wao aliyepo hapa kuomba watusaidie. Wamekubali kufanya hivyo, hatua iliyobaki ni kuwasilisha maombi rasmi kupitia njia za kidiplomasia ili watusaidie kupitia taasisi yao ya Thailand International Cooperation Agency.

By Jamhuri